Klabu zitumie dirisha dogo la usajili kwa faida

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI -

DIRISHA dogo la usajili linatarajia kufunguliwa Jumatano wiki ijayo likihusisha klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu na Daraja la Kwanza Tanzania Bara.

Kipindi cha mwezi mmoja kitakuwa kwa klabu kufanyia kazi ripoti zilizowasilishwa na makocha wa timu zinazoshiriki ligi hiyo, kutokana na mahitaji ya kuboresha vikosi vyao.

Dirisha dogo la usajili linatarajia kufunguliwa baada ya kila timu kucheza michezo tisa katika mzunguko wa kwanza wa ligi.

Ni wazi kwamba klabu zinatarajia kuingia sokoni kusajili baada ya makocha wao kuona upungufu uliomkwamisha kupata matokeo mazuri na sasa akihitaji kutumia kipindi hiki kwa faida kwa kusajili wachezaji ambao watakuwa na msaada mkubwa kwa timu.

Tayari baadhi ya makocha wameanza kusajili kimya kimya ili kuepuka hujuma ambazo wanaweza kufanyiwa na wapinzani wao.

Nikianzia Ligi Kuu, klabu zinatakiwa kuzama kufanya usajili wa maana kutokana na ushindani uliopo katika kuwania taji la msimu huu. Lakini ushindani ambao unaonekana kwenye Ligi Daraja la Kwanza ni wazi kwamba klabu zinatakiwa kufanya usajili utakaolenga kuwapatia matokeo mazuri, ili timu hizo ziweze kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Sasa usajili mdogo utaziwezesha klabu kufanyia marekebisho sehemu ya mapungufu ambayo yameonekana tangu kuanza kwa ligi hizo ili kuweza kupata ushindi katika kila mchezo. Kikubwa kinachohitajika

ni mabenchi ya ufundi ya kila timu kuangalia umuhimu wa kuongeza wachezaji wenye viwango vya hali ya juu na si bora mchezaji.

Lakini viongozi wa klabu hizo wanatakiwa kufanya usajili kwa kuzingatia ripoti ya makocha wa timu zao, kwa kuwa wao ndio wanaojua upungufu katika vikosi vyao na mchezaji ambaye anamhitaji asajiliwe.

Tumesikia mara kadhaa baadhi ya makocha wakilalamika kwamba wanaingiliwa majukumu yao na viongozi wa klabu kuanzia usajili wa wachezaji, kwani wamekuwa wakisajili wachezaji ambao hawakuwa katika mapendekezo ya ripoti zao.

Kibaya zaidi timu inapofanya vibaya lawama zote zinakwenda kwa kocha, hivyo ni bora viongozi wakabaki katika kuweka sera ya klabu huku masuala ya kiufundi yakibaki kwa mabenchi ya ufundi.

Tunatambua kuwa tayari klabu zote zilifanya usajili wa kuridhisha mwanzoni mwa msimu na kipindi hiki ni kuangalia tu pale penye mapungufu kidogo na kufanyia marekebisho na si kuanza tena kufumua kikosi kizima, kwani kufanya hivyo ni sawa na kujitafutia matatizo zaidi.

Klabu kama Simba na Singida United zimeonekana kufanya usajili wa gharama, hivyo hatutegemei mabadiliko makubwa ndani ya vikosi vyao zaidi ya kupunguza ama kuongeza wachezaji wachache wenye manufaa kwa timu.

Naamini kila shabiki anatamani kuona mafanikio katika timu yake, hivyo kipindi hiki cha usajili mdogo viongozi watulize akili na kusajili wachezaji kutokana na mahitaji ya makocha wa klabu hizo.

Kwenda kinyume na mahitaji ya kocha kunaweza kuivuruga timu ambayo katika kipindi hiki cha usajili kilihitaji kufanya maboresho kidogo.

Katika hilo viongozi wa klabu wanatakiwa kubadilika kwa kuzingatia mapendekezo yanayowasilishwa na mabenchi ya ufundi kusajili wachezaji ili kuweza kutengeneza vikosi bora.

Ni imani yangu kwamba kila klabu itafanya usajili kwa wakati kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo Desemba 15, mwaka huu.

Katika hilo viongozi wa klabu wanatakiwa kubadilika kwa kuzingatia mapendekezo yanayowasilishwa na mabenchi ya ufundi kusajili wachezaji ili kuweza kutengeneza vikosi bora.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.