NDEMLA AKIFUZU, WA KWANZA KUFURAHI ATAKUWA KOPUNOVIC

Bingwa - - UCHAMBUZI -

Kopunovic ambaye alirithi mikoba ya Zdravko Logarusic, alikuwa akiuhusudu sana uwezo wa Ndemla na hata alipokuja Dylan Kerr, bado naye alimtumia vilivyo kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali mpaka alipoondoka.

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Said Ndemla, amekwenda Sweden katika timu ya AFC Eskelistuna kwa majaribio ya siku 14 na kama bahati itamwangukia, atafuata nyayo za watangulizi wake akiwamo Mbwana Samatta aliyekipiga nchini Ubelgiji.

Safari ya Ndemla kwenda kufanya majaribio ilikuwa ikitajwa tangu mwaka juzi, ambapo Rais wa Simba, Evance Aveva, alisema kiungo huyo na aliyekuwa beki wa kati wa kikosi hicho, Hassani Isihaka, walikuwa wakihitajika moja ya timu ya Hispania.

Hata hivyo, timu ya Sweden iliongelewa siku nyingi mpaka ikafika hatua hata Ndemla mwenyewe akakata tamaa, lakini sasa Mungu amenyoosha mkono wake na kijana huyo amefika nchini humo na kilichobakia ni kuanza majaribio yake.

Ndemla ni kijana aliyekulia Simba katika kikosi B na baadhi ya wenzake walioanza kuaminiwa na kupandishwa kikosi cha kwanza na aliyekuwa kocha mkuu Patrick Liewig, alipoamua kuanza kuwatimua wachezaji wakongwe aliowaona wanampotezea muda.

Kati ya makocha ambao Ndemla alifaidi ni Goran Kopunovic, ambapo ilikuwa nadra sana kumwona akianzia benchi na kocha huyo anaweza kupata faraja kubwa akisikia kijana wake aliyekuwa akimpenda, amepata bahati ya kwenda kufanya majaribio nchini Sweden.

Kopunovic ambaye alirithi mikoba ya Zdravko Logarusic, alikuwa akiuhusudu sana uwezo wa Ndemla na hata alipokuja Dylan Kerr, bado naye alimtumia vilivyo kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mashuti makali mpaka alipoondoka.

Aliyekuja kumuumiza Ndemla ni Jackson Mayanja, kwani baada ya kupokea mikoba kukaimu nafasi ya ukocha mkuu, alianza kumweka benchi kiungo huyo na mara nyingine kutokumpa kabisa nafasi hadi ikafika hatua akatemwa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Hakuna ubishi kwamba Mayanja ni moja ya makocha waliosababisha uwezo wa Ndemla kuanza kuporomoka, kwani hakuwa na mipango naye kabisa na hata alipokuja Joseph Omog, bado kiungo huyo alikuwa kwenye wakati mgumu, lakini sasa tunamwombea mambo yamnyookee huko alikokwenda.

Ninaamini kwamba kama leo Omog angefukuzwa Simba na Ndemla akaambiwa achague kocha atakayerithi mikoba yake, bila kigugumizi angewashauri kumrudisha Kopunovic, kwani ni moja ya makocha wanaohusudu viwango vya wachezaji chipukizi.

Ni kocha ambaye anaheshimu kila mchezaji ndiyo maana wakati ule alipoachana na Simba baada ya kushindwana kwenye nyongeza ya fedha ili aongeze mkataba, baadhi ya wachezaji nadhani akiwamo Ndemla, walikosa ujasiri lakini hawakuwa na namna ya kufanya.

Nakumbuka kocha wa zamani wa kikosi hicho, Logarusic, wakati anasaini timu ya Asante Kotoko ya nchini Ghana, nilimuuliza akipata nafasi ya kusajili mchezaji kutoka Tanzania, angemchukua nani, alinijibu kwamba Ndemla ni moja ya wachezaji anaowahusudu na angependa kufanya naye kazi.

Kilichomzuia Logarusic kumsajili Ndemla ni kwamba, alifikia katika timu hiyo dirisha la usajili likiwa limefungwa ila aliahidi kufanya kila linalowezekana dirisha jingine likifunguliwa atamchukua, lakini bahati mbaya sana akatimuliwa kwenye timu ikiwa imecheza michezo michache.

Ndemla alikuwa kipenzi cha baadhi ya makocha waliopita katika kikosi hicho isipokuwa Mayanja pekee na wala hatuwezi kumlaumu sana Mganda huyo, kwani kila kocha analo chaguo na mipango yake japo kwa namna moja ama nyingine kama angeendelea kuwepo ni wazi angezika kipaji cha kiungo huyo.

Ndemla ni mchezaji ambaye hana makuu kama baadhi ya wachezaji wenzake, kwani anazungumza vizuri na kila mtu. Baadhi ya wachezaji akisajiliwa na timu hizi kubwa za Simba na Yanga, anajiona yeye ni kila kitu, lakini Ndemla si mmoja wa hao.

Nina uhakika kama Kopunovic angeendelea kuifundisha Simba kwa muda mrefu, bila shaka kiwango cha Ndemla kingekuwa juu zaidi ya hapo kilipo na huenda leo hii angekuwa amepata timu nje ya Tanzania, ila tuishie tu kusema kila jambo na wakati wake.

Kilichobakia ni kupiga magoti kumwombea Ndemla afuzu majaribio ili Tanzania iongeze idadi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje, kwani matunda yake tutayaona litakapokuja suala la kuichezea timu ya Taifa.

Kwa sasa wachezaji ambao tunawategemea zaidi ni akina Mbwana Samatta, anayechezea Genk ya Ubelgiji, Abdi Banda anayecheza Afrika Kusini na Simon Msuva anayecheza Morocco, sasa akiongezeka Ndemla, itakuwa faida kubwa kwa Taifa. Mungu mbariki Ndemla.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.