Klabu zinawapima wachezaji kweli kabla ya kuwasajili?

Bingwa - - UCHAMBUZI -

WAHENGA walisema mazoea hujenga tabia na hili tumeendelea kuliona kwa klabu zetu za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Tatizo hilo ni moja ya matatizo sugu yaliyopo kwenye klabu zetu hapa nchini na limekuwa hivyo kwa miaka mingi bila kupata dawa.

Imekuwa ni kawaida kwa klabu hasa kubwa kusajili wachezaji na baadaye kwenda kupima afya, kitu ambacho kinatokea Tanzania peke yake.

Mpaka sasa timu za ligi kuu zimecheza michezo tisa kati ya michezo 15 wanayotakiwa kucheza, lakini kuna wachezaji ambao hawajacheza mchezo hata mmoja na wengine wamecheza michache kwa sababu ya majeraha ambayo yamekuwa yakiwasumbua mara kwa mara.

Kabla ya msimu huu kuanza tuliona Klabu ya Yanga ikiendesha zoezi la upimaji wa afya kwa wachezaji wake ambalo lilifanyika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salam, wakiwa na jopo la madaktari.

Timu hizo zimekuwa na mbwembwe nyingi na si Yanga tu, wamo pia Simba na Azam FC ambao wamekuwa wakisajili kwa kupiga lamri na mwisho wa siku zimekuwa zikiingia hasara kubwa.

Tumezoea kuiga kila kitu kutoka kwa wenzetu Ulaya waliotutangulia kisoka, lakini tumeshindwa kuiga hilo. Yaani tunawadharau walimu wetu na kujiona sisi ndio tunajua zaidi.

Mara nyingi tumekuwa tukisikia wachezaji wanapimwa afya na picha tunaziona anavyopimwa kila kitu, na mwisho wa siku wanaingia naye mkataba kama wameona yupo vizuri, lakini kwetu tunaingia mkataba kwanza na baadaye tunawapima afya, tena tunawapima kifua na malaria hapo tumemaliza.

Halafu baadaye wanadanganya kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kupeleka vyeti vya vipimo feki, kwa sababu kanuni zinawataka klabu kuwapima afya wachezaji kabla ya kuwasajili.

Ndio maana leo tunaona wachezaji kama Shomary Kapombe, Said Mohamed ‘Nduda’ John Bocco ‘Simba’ na Amis Tambwe na Dolnad Ngoma ‘Yanga’ ambao wote wamesaini mikataba mipya na klabu hizo, wakiwa nje kwa muda mrefu kwa sababu ya majeraha.

Hawa wachezaji wamesajili wakati klabu zao zinajua kwamba ni majeruhi na wengine wanatakiwa kupata matibabu makubwa na ya muda mrefu, lakini bado waliwasajili kwa kauli za kuwa wamepona na sasa wapo fiti nadhani nao waliwapima kwa macho, bila kufuata vipimo vya wataalamu.

Klabu hizo zimekuwa na ubabaishaji mwingi kwenye kila kitu na wamekuwa chanzo kikubwa cha kulibomoa soka la Tanzania kwa makusudi bila hata huruma.

Wanachofanya ni kiini macho kwa wanachama na mashabiki wao, waone kuwa taratibu zinafuatwa wakati hakuna kitu, inakuwa ni ‘danganya toto’.

Mfano mzuri ni kwa timu ya Simba ambao ilimsainisha mkataba kiungo Mkenya Paul Kiongera, ambaye awali alikuwa akicheza katika timu ya KBC ya Kenya.

Viongozi wa timu ya Simba na jopo la madaktari kwa ujumla walikuwa hawana muda wa kumchukua vipimo mchezaji huyo kwa kuamini yupo fiti kwa asilimia 100, kumbe mchezaji huyo anasumbuliwa na tatizo la goti.

Utaona jinsi gani viongozi wetu wa soka wanavyokosa umakini katika suala la kuzingatia afya za wachezaji wao, pia hata wachezaji nao hawapo makini katika kuzingatia afya zao.

Nchi hii katika soka kumejaa viongozi wababaishaji ambao hawana vipaji vya kweli katika kuongoza mpira na ndio maana ubabaishaji unazidi badala ya kupungua, umefika wakati nao waone aibu kulitumikia na kuliongoza soka kikamilifu.

Wachezaji hao wafike wakati waache tamaa zisizo na faida kwao, waangalie afya zao kwanza maana wakiwa na afya njema wanaweza kupata vinono zaidi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.