SIMBA YAMPASUA KICHWA TSHISHIMBI

Bingwa - - MBELE - NA TIMA SIKILO

KITENDO cha Simba kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kumbe hakiwaumi mashabiki peke yao kwani hata wachezaji hawapati usingizi kabisa na badala yake wanatunga mbinu namna ya kuwashusha wapinzani wao hao wa jadi.

Kiungo wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Pappy Kabamba Tshishimbi, hatamani kabisa kuangalia msimamo kwani unamtia kichefuchefu anapowaona Simba wapo juu.

Akizungumza na BINGWA jana, Tshishimbi alisema kitendo cha simba kuongoza ligi kinawaumiza sana vichwa, na tayari wameshaweka mipango ya kuhakikisha wanawapiga chini na wao kurudi kwenye nafasi yao.

“Tangu ligi imeanza simba wamekuwa kileleni jambo ambalo sisi kama timu haturidhishwi nalo, kwa kweli hili linatuumiza sana, lakini tunaamini muda si mrefu tutaichukua hiyo nafasi kwani tumeamua kupambana mpaka kieleweke,” alisema Tshishimbi.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba wanaongoza wakiwa na pointi 19, sawa na Azam FC, wanaoshika nafasi ya pili timu hizo zikipishana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Yanga wakishika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 17. Kitendo hicho ndicho kinachomuuma Tshishimbi ambaye ameweka bayana kwamba anatamani kuiona Yanga ikiwashusha haraka sana wapinzani wao hao wa jadi ili kuwakata kidomodomo chao.

Kikosi cha Yanga kinaendelea na mazoezi yao katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, chini ya kocha wao msaidizi Shedrack Nsajigwa, wakijiandaa na mchezo wao dhidi ya Mbeya City, unaotarajiwa kuchezwa Novemba 19, uwanja huo wa Uhuru.

Timu hizo kila moja imecheza michezo tisa na zinatarajiwa kushuka tena uwanjani mwishoni mwa wiki ijayo, ambapo wakati Yanga wakiwakabili Mbeya City, Simba wao wanatafuta namna ya kuondoka na pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons mchezo utakaochezwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.