KUTINYU YANGA, NGOMA SINGIDA

Singida United wataja dau, Mkwasa afunguka

Bingwa - - MBELE - HUSSEIN OMAR NA CLARA ALPHONCE

ZIKIWA zimebaki siku tano kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa, Yanga imenasa kwa mshambuliaji wa Singida United raia wa Zimbabwe, Tafadzwa Kutinyu, ili kuboresha kikosi chao kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani, lakini pia kutetea ubingwa wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Na baada ya kuvutiwa na straika huyo inayemwona ndiye anayeweza kuunda kombinesheni hatari pamoja na Ibrahim Ajib na Obrey Chirwa, Yanga inafanya kila liwezekanalo kumsajili Mzimbabwe huyo.

Chanzo cha ndani kutoka Yanga kimeeleza kuwa klabu hiyo inajiandaa kutuma maombi yao hayo Singida United na kwamba, wapo tayari kubadilishana nao kwa kuwapa kati ya washambuliaji wao wawili, Mzimbabwe Donald Ngoma au Amissi Tambwe raia wa Burundi.

Uzuri ni kwamba washambuliaji wote hao walisajiliwa chini ya utawala wa Hans nav der Pluijm aliyekuwa kocha wa Yanga ambaye kwa sasa anainoa Singida United, hivyo ni wazi angependa kukumbushia maisha ya awali dhidi ya mmoja wa wawili hao au wote kama ikiwezekana.

Katika kuthibitisha uhitaji wao wa Kutinyu, kiongozi mmoja wa Yanga aliliambia BINGWA kwamba: “Tulimwona mchezaji huyo tulipocheza na Singida, akicheza na Ajib pamoja na Chirwa pale kati, wanaweza kufanya vizuri kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha. Kwa sasa tunatafuta mshambuliaji wa kati na wingi pamoja na beki wa kati.”

Alipoulizwa juu ya mpango huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Singida United, Festo Sanga, alisema wapo tayari kumwachia Kutinyu kwa dau la Dola za Marekani 100,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 200 kwa timu za Tanzania na kwa timu za nje ni Dola 150,000 (Sh mil 300).

Alisema mbali ya Yanga, kuna klabu nyingine za nje zimeonyesha kuvutiwa na mchezaji huyo, ikiwamo Orlando Pirates ya Afrika Kusini inayonolewa na Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ na nyingine ya Ujerumani.

“Mpaka sasa tumepokea ofa nyingi sana kutoka klabu mbalimbali, si kwa Yanga tu, kama hao Orlando wapo tayari kutoa fedha hiyo lakini bado tunafikiria,” alisema Sanga.

Alipoulizwa kuwa wapo tayari kumwachia Kutinyu wabadilishane na Ngoma ambaye ni kipenzi cha Pluijm au Tambwe, alisema: “Ngoma hana hadhi ya kuichezea Singida United.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, akilizungumzia suala hilo, alisema kuwa hawezi kuliweka wazi moja kwa moja kwa kuwa bado hana taarifa nalo, ila kama lipo kamati husika italiweka wazi.

Alisema wao mpaka sasa wana nafasi moja ya kujaza kwa wachezaji wa nje, wanaangalia jinsi ya kuijaza kutokana na umuhimu wa nafasi yenyewe

Pamoja na kuibeba Yanga msimu uliopita, msimu huu Ngoma na Tambwe wameshindwa kuisaidia timu hiyo kutokana na kuandamwa na wimbi la majeraha na hivyo kujikuta wakisotea benchi.

Kutinyu Ngoma

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.