Simba yapewa straika hatari

Akitua Msimbazi, mtamkoma Niyonzima

Bingwa - - MBELE - NA SAADA SALIM

WAKATI benchi la ufundi la Simba likipendekeza kusaka straika ambaye atatengeneza kombinesheni nzuri na Emmanuel Okwi katika safu ya ushambuliaji, tayari kiungo wa zamani wa timu hiyo, Pierre Kwizera, amewapa viongozi wa klabu hiyo majina ya mastraika hatari anaoamini watawasaidia Wekundu wa Msimbazi hao.

Wachezaji hao ni Mkongo Papy Kamanzi kutoka Intecelles FC, Nahimana Shassir na Ismala Diarra wanaokipiga katika klabu ya Rayon Sport, zote zikishiriki Ligi Kuu ya Rwanda.

Kwizera ameliambia BINGWA jana kwamba kwa jinsi alivyoiona Simba wakati wa tamasha la `Simba Day`, ni timu nzuri, lakini bado inahitaji mtu ambaye atacheza vizuri na Okwi na kupata idadi kubwa ya mabao.

Alisema Simba kama inatafuta straika ni dhahiri kuwa miongoni mwa wachezaji hao akiwamo Kamanzi ambaye anaongoza kwa ufungaji mabao Rwanda, ataisaidia timu hiyo.

“Hao wote niliotaja ni wachezaji wazuri, naamini watakuwa ni msaada na kukidhi kile wanachohitaji Simba katika kuimarisha safu yao ya ushambuliaji na hatimaye kutwaa ubingwa na kufanya vizuri kimataifa,” alisema.

Kiungo huyo alisema hata kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, anafahamu uwezo wa Diarra na Shassir kwani aliwafundisha.

“Hao wachezaji wawili wametoka mikononi mwa Irambona (Djuma), anawafahamu vizuri, kuhusu Papy amemwona katika ligi ya Rwanda, hivyo endapo mmoja anaweza kuchukuliwa na kutumiwa ipasavyo, basi Simba itakuwa imeimarika zaidi,” alisema.

Alipoulizwa iwapo wataufanyia kazi ushauri huo wa Kwizera, Katibu Mkuu wa Simba, Arnold Kashembe, alisema mchakato wa usajili unaendelea na kama kuna mchezaji atakuja kufanya majaribio kwao, hawana shida.

“Kamati yetu ya usajili inakutana wikiendi hii kwa ajili ya kuangalia mapendekezo ya mwalimu na sehemu za kusajili, kwani ukiangalia kwa sasa kikosi chetu ni kipana,” alisema.

Kashembe alisema licha ya upana wa kikosi chao, bado watafanya marekebisho madogo katika baadhi ya nafasi ambazo kocha huyo anazihitaji kwa ajili ya ligi na michuano ya kimataifa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.