ULIMWENGU ATUA YANGA

SASA AJIB KAMA ANAMSUKUMA MLEVI, CHIRWA KAMA ANANAWA VILE

Bingwa - - MBELE -

WAKATI dirisha dogo la usajili Ligi Kuu Bara likitarajiwa kufunguliwa keshokutwa, Yanga iko mbioni kumsajili mshambuliaji wa zamani wa TP Mazembe ya Congo...

HUSSEIN OMAR NA ABDUL MKEYENGE

WAKATI dirisha dogo la usajili Ligi Kuu Bara likitarajiwa kufunguliwa keshokutwa, Yanga iko mbioni kumsajili mshambuliaji wa zamani wa TP Mazembe ya Congo, Mtanzania Thomas Ulimwengu.

Ulimwengu anayekipiga kwenye klabu ya Athletic Football Club Eskilstuna ya Sweden, anatua Yanga kwa mkataba wa miezi sita ili kurejesha kiwango chake baada ya kutoka kwenye majeraha ya goti.

Mshambuliaji huyo kwa sasa yupo katika mazoezi maalamu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya kurejea uwanjani kuitumikia Yanga katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa mwakani.

Na iwapo dili hilo litakamilika, ni wazi kuwa washambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib pamoja na Obrey Chirwa, watakuwa ni kama ‘wanamsukuma mvevi’ kwani hawatakuwa na kazi kubwa ya kupambana na mabeki wa timu pinzani wakimwachia Ulimwengu ambaye shughuli yake si ya kitoto.

Pamoja na uwezo wa hali ya juu alionao Ulimwengu katika soka, lakini pia anabebwa na nguvu zinazomwezesha kupambana na mabeki watemi kama Method Mwanjali wa Simba na wengineo, hivyo kuwafanya akina Ajib kubakiwa na kazi moja tu ya kucheka na nyavu.

Chanzo cha ndani kutoka Kamati ya Usajili Yanga, kimelidokeza BINGWA kuwa, Ulimwengu amepewa miezi sita ya kutafuta timu ya kurejesha makali yake na baadaye aweze kurejea klabuni kwake.

“Tuko kwenye mazungumzo ya kumwongeza Ulimwengu katika kikosi chetu. Kama unavyojua, tutashiriki michuano ya kimataifa mwakani, hivyo unavyokuwa na mshambuliaji kama Ulimwengu, unakuwa na mtu mwenye faida ndani ya kikosi.

“Mazungumzo yamefikia sehemu nzuri juu ya Ulimwengu kuja kujiunga nasi na kama unavyojua, dirisha lenyewe linafunguliwa wiki ijayo (Jumatano), hivyo lolote linaweza kutokea ndani ya siku hizi mbili,” alisema mtoa habari wetu huyo wa uhakika.

Kwa muda mrefu, Yanga ilikuwa ikimwinda mshambuliaji huyo kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake.

Ujio wake ndani ya Yanga katika kipindi cha dirisha hili dogo la usajili, utakuwa faraja kwa mashabiki wa timu hiyo ambao msimu huu wameshindwa kupata huduma ya washambuliaji wao, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wanaokabiliwa na majeraha.

BINGWA lilipowatafuta viongozi wa juu wa klabu hiyo ili kupata uthibitisho wa taarifa hizi, kila mmoja alitoa majibu tofauti.

Katibu Mkuu Yanga, Charles Mkwasa, alisema taarifa hizo ni njema, lakini kwa sasa yuko ‘bize’ na atazitolea ufafanuzi baadaye.

“Tumefurahishwa na taarifa hizi kama klabu, lakini kwa sasa ni mapema kuzitolea ufafanuzi wowote ule. Niache kidogo niko bize,” alisema Mkwasa.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga, alisema lolote linaweza kutokea na kusisitiza kuwa yupo safarini hawezi kulitolea zaidi ufafanuzi suala hilo.

“Nipo safarini, lolote linaweza kutokea, lakini kwa sasa siwezi kulizungumzia hilo,” alisema Sanga.

Licha ya Ulimwengu kutajwa kujiunga na Yanga, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mzambia George Lwandamina, anarejea nchini leo akitokea mapumzikoni nchini kwao na anatarajiwa kuja na kiungo mshambuliaji raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.