SAID NDEMLA KUANZA MAJARIBIO ULAYA LEO

Bingwa - - HABARI/MATANGAZO -

NA ABDUL MKEYENGE

KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Simba, Said Ndemla, leo anatarajia kuanza majaribio ya wiki mbili katika klabu ya AFC Eskilstuna ya nchini Sweden.

Ndemla aliondoka nchini wiki iliyopita kwenda kujaribu bahati yake ya kucheza soka la kulipwa, ambapo kama atafuzu majaribio ataungana na mshambuliaji, Thomas Ulimwengu anayeichezea timu hiyo.

Ndemla atafanya majaribio katika uwanja wa timu hiyo Tunavallen na kusimamiwa na benchi la ufundi lililopo chini ya kocha, Michael Jolley.

Akizungumza na BINGWA, kiungo huyo alisema amefika salama nchini Sweden na leo ataingia rasmi uwanjani kujaribu bahati, ambapo amewataka Watanzania wamwombee.

Alisema tayari ameshapewa vifaa vya majaribio na anachosubiri ni kuingia uwanjani kuonyesha uwezo wake ili abaki nchini humo.

“Nimejiandaa vema na kesho (leo) nitaanza majaribio, nawaomba Watanzania waniombee nifanye vizuri ili niweze kubaki huku.

“Jamaa wako makini sana na mambo yao kwani wameshanipa kila kitu ambacho napaswa kukitumia uwanjani, sasa ni jukumu langu kuwaonyesha nilichonacho,” alisema Ndemla.

Kiungo huyo aliongeza kuwa hali ya hewa ya baridi nchini humo haimsumbui sana, kwa kuwa anaamini anapokuwa kazini hapaswi kujali kitu zaidi ya kufanya vema.

“Hali ya hewa ni baridi kali inayotufanya watu ambao hatujazoea mazingira tukae ndani muda mrefu, lakini binafsi sioni kama hali hiyo ni tatizo sana, kikubwa nimejiandaa kufanya vizuri katika majaribio,” alisema Ndemla.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.