Kocha Mbao ataka vifaa viwili Yanga

Bingwa - - HABARI/MATANGAZO -

NA WINFRIDA MTOI

KOCHA mkuu wa timu ya Mbao FC, Ettiene Ndayiragije, ameweka wazi kuwa anawahitaji wachezaji wawili wa Yanga kwa mkopo ili kukiongezea nguvu kikosi chao.

Mrundi huyo anawataka wachezaji Makka Edward na Yussuf Mhilu ambao hawapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha kocha Mzambia, George Lwandamina, ili awasajili katika dirisha dogo litakalofunguliwa keshokutwa.

Ndayiragije amepanga kuwanasa nyota hao ili kukiimarisha kikosi chake ambacho kiliondokewa wachezaji kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu.

Edward na Mhilu walipandishwa kucheza timu kubwa kutoka katika kikosi cha vijana lakini hawajapata namba za kudumu kikosi cha kwanza.

Akizungumza na BINGWA jana, Ndayiragije alisema kwa sasa anasubiri majibu kutoka kwa uongozi wa klabu ya Yanga kwani anawahitaji sana wachezaji hao katika kikosi chake.

“Kuna idara zinahitaji kuongezewa nguvu katika kikosi, lakini nasubiri kukaa na uongozi baada ya mechi ili kujua cha kufanya, Makka na Mhilu ni wachezaji wadogo wenye uwezo, hivyo Yanga wakikubali itakuwa vizuri ingawa kuna wengine nawataka kutoka timu nyingine,” alisema.

Akizungumzia suala hilo Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa, alisema ni kweli wamepata maombi hayo na hawana tatizo la kuwatoa wachezaji hao bali ni lazima kocha aridhie kama hawapo kwenye programu yake.

“Tumepokea barua nyingi za kuombwa wachezaji, lakini tunamsubiri mwalimu ili aweke wazi wachezaji anaowahitaji kikosini, kama hawa wanaotakiwa hawapo kwenye programu yake basi tutawaruhusu kuondoka hakuna tatizo,” alisema Mkwasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.