Katwila atunisha msuli kwa Mexime

Bingwa - - HABARI/MATANGAZO -

NA WINFRIDA MTOI

KOCHA mkuu wa timu ya Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, ameeleza kuwa hana hofu yoyote kuelekea katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, huku akisisitiza kwamba kila mmoja atapambana na hali yake.

Makocha wanaovinoa vikosi hivyo, waliwahi kufanya kazi pamoja wakiwa Mtibwa ambapo Mecky Mexime anayeifundisha Kagera kwa sasa alikuwa kocha mkuu, huku Katwila akiwa msaidizi wake.

Vikosi vya makocha hao vitashuka dimbani wikiendi hii kuvaana katika mchezo wa Ligi Kuu ukiwa ni msimu wa pili mfululizo kukutana kila mmoja na timu yake.

Akizungumza na BINGWA jana, Katwila alisema anaamini mchezo utakuwa mzuri kwani wakikutana kila mmoja anapambana kivyake kutokana na namna alivyojipanga.

“Ni mechi inayowavutia mashabiki wa timu zote mbili, kila mmoja anajiandaa kupata ushindi kwani kinachotakiwa ni matokeo mazuri.

“Mara nyingi tukianza kuwafunga Kagera katika Uwanja wa Manungu tukienda kucheza katika uwanja wao wa Kaitaba pia tunawafunga,” alisema Katwila.

Msimu uliopita Mtibwa waliwafunga Kagera mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Manungu, Morogoro na walivyorudiana katika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba walishinda mabao 2-1.

Kwa sasa Mtibwa imejiimarisha katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 17, wakati Kagera wanashika nafasi ya 13 wakiwa na pointi saba, zote zikiwa zimeshuka dimbani mara tisa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.