Maguli agoma kurejea Bongo

Bingwa - - HABARI/MATANGAZO -

NA ZAINAB IDDY

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Dhofar SC ya nchini Oman, amesema ni bora astaafu kuliko kurejea nchini kucheza soka.

Straika huyo hana mpango wa kurudi Bongo akidai kwamba ni zilipendwa, hivyo kama atashindwa kuendelea kucheza nje ya nchi ni heri kustaafu.

Maguli alijiunga na klabu ya Dhofar SC inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini Oman kwa mkataba wa miaka mitatu, ambapo tayari ameshaitumikia timu hiyo kwa misimu miwili sasa. Akizungumza na BINGWA, Maguli alisema tangu awali aliweka sawa mipango yake kuwa akipata nafasi ya kucheza soka la kulipwa hatarudi nyuma, hivyo hafikirii kucheza tena soka hapa nchini.

“Mkataba wangu na klabu ya Dhofar unamalizika msimu ujao, lakini tayari kuna mipango inafanyika ambayo itakuwa na machaguo matatu.

“Kama mipango hiyo itakwenda vizuri, nitakwenda kucheza soka la ushindani katika timu nyingine itakayoonyesha nia ya kunihitaji, lakini ikishindikana nitaongeza mkataba.

“Kama yote haya hayatatimia basi maisha yangu ya kucheza soka yatakuwa yamefika mwisho, hivyo nitaangalia jambo lingine la kufanya kwenye soka lakini si kurudi tena nyuma,” alisema Maguli.

Maguli alieleza kuwa kuna timu tatu zimeonyesha nia ya kumhitaji, ambapo moja ni ya nchini Oman na nyingine Ufaransa, hivyo zinasubiri amalize mkataba ili waanze mazungumzo kutokana na klabu yake ya Dhofar kukataa kumuuza.

“Ilikuja ofa kutoka nchini Ufaransa mwishoni mwa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Oman, lakini sikuweza kwenda kwa sababu timu iliyonihitaji ilishindwa kuvunja mkataba wangu na Dhofar, hivyo kuamua kusubiri hadi umalizike,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.