Thamani ya mchezaji isiishie kwenye benchi

Bingwa - - MTAZAMO MAONI KATUNI -

Tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakiridhika kukaa benchi muda mrefu hata msimu mzima kisa wanacheza katika timu kubwa bila kujali kuwa vipaji vyao vinapotea.

DIRISHA dogo la usajili Tanzania Bara linatarajia kufunguliwa keshokutwa, ambapo klabu zinajipanga kuviimarisha vikosi vyao kutokana na upungufu ulionekana katika michezo tisa iliyochezwa.

Klabu 16 zinazoshiriki ligi kuu na 24 zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara zinajiandaa kuingia sokoni kusajili wachezaji wapya kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi katika vikosi vyao.

Tayari tetesi za wachezaji wanaoondoka katika klabu zao na kwenda kujiunga na nyingine zimeanza kuvuma kabla ya dirisha lenyewe kufunguliwa rasmi Jumatano.

Hiki ni kipindi kingine cha mavuno kwa wachezaji ambapo kila mmoja anahitaji kusajiliwa na klabu ambayo itampa manufaa makubwa katika maisha yao.

Ni kipindi ambacho wachezaji hawatakiwi kufanya makosa, kwani ni usajili wa mwisho kwa Ligi ya Tanzania Bara kabla ya kufikia msimu wa dirisha kubwa mwakani.

Kwa maana ya wachezaji wa timu hizo ni kipindi cha kujitafakari na kufanya uamuzi sahihi kwa klabu itakayowahitaji ili waweze kusajiliwa na kuendeleza vipaji vyao.

Kabla ya kuweka dole gumba kwa mchezaji, ni lazima ajue klabu itakayomhitaji kama atakuwa na nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza ili asifikie kakaa kwenye benchi kwa kipindi chote cha makubaliano ya mkataba wao.

Tunajua wapo wachezaji tangu wamesajiliwa wakati kama huu hawajapata nafasi ya kucheza hata mechi moja ya ligi zaidi ya zile za kirafiki kutokana na ushindani wa namba.

Wachezaji wengi wamejikuta wakishuka viwango kutokana na kusota kwenye benchi na kupoteza kabisa vipaji vyao walivyoibuka na klabu walizotoka.

Haiwezekani mchezaji amekaa nusu msimu hajacheza mechi yoyote ya mashindano halafu anaendelea kukaa katika klabu ambayo haimtumii, eti kwa sababu ya masilahi huku kipaji chake kikiendelea kudidimia.

Wachezaji kama hao wapo zaidi kwenye timu kubwa ambazo zina nyota wengi wenye uwezo, ikiwamo wa kigeni wanaopewa kipaumbele cha kucheza, hivyo inakuwa ni ngumu kwa mchezaji wa kawaida kupata namba kiurahisi hata kama alikotoka alikuwa anang’ara.

Ili mchezaji aendelee kuwa katika kiwango ni lazima anapotoka timu moja kwenda nyingine apate nafasi ya kucheza kama ilivyokuwa awali, tofauti na hapo thamani ya mchezaji inaishia kwenye benchi la wachezaji wa akiba.

Tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakiridhika kukaa benchi muda mrefu hata msimu mzima kisa wanacheza katika timu kubwa bila kujali kuwa vipaji vyao vinapotea.

Wapo wanaogoma kabisa kutolewa kwa mkopo katika klabu nyingine kwa lengo la kukuza viwango vyao na matokeo yake wanaendelea kusotea namba na baadaye vipaji kupotea.

Ifahamike kuwa hakuna klabu yoyote inayoweza kuchukua mchezaji ambaye haonekani alichokifanya kwa msimu mzima wa ligi.

Mfano mzuri wa wachezaji ambao wameona faida ya kujiunga na klabu nyingine ni kipa wa Simba, Manyika Peter, alikokuwa anasugua benchi kwa muda mrefu na kwenda Singida United, ambako kiwango chake kimerudi na kuitwa kwenye kikosi cha Taifa, Taifa Stars.

Kutokana na hilo, ni jukumu la wachezaji wengine kuthamini vipaji vyao kwa kuanza kuchangamkia nafasi za kwenda kucheza kwa mkopo katika timu zinazowahitaji au kama kuna uwezekano wakuvunja mikataba ili wakacheze katika timu nyingine wanayoiona wanapata nafasi ya kucheza.

Leo hii Manyika Jr, kama angeendelea kung’ang’ania kukaa Simba, sidhani kama kocha wa timu ya taifa angeshawishika kumuita kwenye kikosi chake.

Kama mchezaji anabaini tangu asajiliwe msimu huu hana namba kwenye kikosi cha kwanza, ni bora akachukua hatua ya kuondoka mapema kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo ili kuokoa kipaji

chake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.