JULIO ALIA BAHATI HAIKUWA YAO

Bingwa - - HABARI -

NA RAMADHAN HASSAN, MPWAPWA

DODOMA FC imepigwa bao 1-0 na Biashara United katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL), iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Mgambo, wilayani Mpwapwa.

Kutokana na matokeo hayo, kocha wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, amesema walikosa bahati ya kupata ushindi, licha ya kutengeneza nafasi 15, lakini wachezaji wake walishindwa kuzitumia.

Moja ya nafasi walizopata ni ile ya Mendy Edward kukosa penalti dakika ya 24, baada ya kipa wa wa Biashara United, Hassan Abdallah, kuokoa.

Lakini washambuliaji wa timu hiyo, Lusajo Laurent na Anwary Awadh, waliongoza kwa kukosa nafasi za wazi za kufunga baada ya mashuti yao kuishia kwa kipa Abdallah.

Akizungumza na BINGWA baada ya mechi hiyo, Julio alisema bahati haikuwa upande wao kushinda, licha ya wachezaji wake kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

"Kweli Mungu yupo, mipira minne imegonga mwamba, siwalaumu wachezaji wangu hii ni hali ya mchezo tu, tunajipanga kwa mchezo unaofuata dhidi ya Alliance School,” alisema.

Biashara United walipata bao dakika ya pili lililofungwa na Kauswa Bernard kwa shuti kali, lililomshinda kipa wa Dodoma, Abdallah Chambala.

Kabla ya kufunga bao hilo, shambulizi lilianzia kwa beki wa kushoto wa timu hiyo, Godfrey Marcus ambaye alipiga mpira mrefu kwa Bernard na kisha kuachia shuti lililotinga wavuni.

Kwa upande wa kocha wa Biashara United, Madenge Omary, alisema licha ya kupata ushindi, mwamuzi alionekana kuwapendelea wenyeji Dodoma lakini Mungu alikuwa upande wao.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.