Kocha New Lige atamba kutwaa taji Arusha

Bingwa - - HABARI -

NA JACKLINE LAIZER, ARUSHA

KOCHA wa timu ya soka ya New Life inayoshiriki Ligi Daraja la Nne ngazi ya Wilaya ya Arusha, Noel Frank, ametamba kuibuka mabingwa wa ligi hiyo .

Akizungumza na BINGWA mjini hapa juzi, Frank alisema kwa ubora wa kikosi chake kimejipanga vizuri, kwani malengo yao ni kuhakikisha msimu ujao wanacheza Ligi ya Mkoa nyingine za juu.

Frank alisema vijana wake wapo vizuri wanajituma na wanafuata maelekezo anayowapa na anaona ubingwa upo kwa timu yake.

“Hatua hii tuliyofikia ya sita bora sioni timu ambayo itatupa shida kwa hiyo ubingwa nauona upo kwa ajili ya timu yangu," alisema Frank.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Taasisi ya New Life, Nicholaus Sawaa, alisema ni mara yao ya kwanza kushiriki ligi hiyo.

Sawaa alisema wana mipango ya kuhakikisha vijana wanaowalea katika soka wanafikia malengo yao ya kuwa wachezaji bora hapa nchini na nje ya nchi.

Alisema anakipongeza kikosi chake kwa kufanikiwa kufika hatua ya sita bora na atahakikisha anaisaidia kwa nguvu zake zote ili iweze kufanya vizuri katika michezo yake na kuchukua ubingwa.

Timu zilizofanikiwa kuingia hatua ya sita bora ni Tanzanite yenye pointi sita, New Life (pointi nne), Bishop Durning School na Arusha City (pointi tatu kila mmoja), Dogo Sammy (pointi moja) na Royal ikishika mkia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.