TUNAMHITAJI KOCHA HERVE RENARD KUINOA TAIFA STARS?

Bingwa - - KOLAMU -

HABARI kubwa ya michezo barani Afrika wiki iliyopita ni kukamilika kwa idadi ya timu tano zilizofuzu kwa fainali za Kombe la Dunia hapo mwakani nchini Urusi.

Usiumize kichwa, Tanzania haimo. Senegal ya Sadio Mane imefuzu. Misri ya Mohamed Salah imefuzu.

Nigeria ya John Obi Mikel imefuzu bila kusahau Tunisia na Morocco ya kocha Herve Renard, nayo pia imefuzu.

Wakati idadi hiyo ikikamilika, Taifa Stars ya Mbwana Samatta, ilikuwa nchini Benin ikijipapatua kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa ugenini mjini Cotonou ambako mimi pia ni sehemu ya watu walioushuhudia mchezo huo nikiwa nchini Benin.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na kocha wetu, Salum Mayanga, lakini bado watu wanaonekana kutoridhishwa na mwenendo wa timu kiujumla.

Tangu Kocha Mayanga aichukue Taifa Stars, mechi yake dhidi ya Benin ilikuwa ni mechi ya 14.

Hapo kabla alikuwa ameiongoza timu kwenye mechi 13 huku akiibuka na ushindi mara tano, akitoka sare mara saba na kupoteza mchezo mmoja pekee. Huyu ni aina ya kocha wakujivunia.

Moja kati ya vitu tunavyojidanganya ni kuamini kwamba tatizo la Stars linatokana na kocha kuwa na uwezo mdogo.

Huku ni kujidanganya mchana kweupe kabisa. Tatizo kubwa la mpira wetu lipo kwenye uongozi unaosua sua k u w e k a ubora wa wachezaji. Renard ni Mfaransa ambaye huenda historia ya soka la Afrika itaendelea kumkumbuka kuliko hata nyumbani nchini Ufaransa.

Ameshinda Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 akiwa na timu ya Taifa ya Zambia, ameshinda tena taji hilo akiwa na timu ya Taifa ya Ivory Coast mwaka 2015 na wikendi iliyopita tumeshuhudia akiwaongoza Morocco na kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast ya Gervinho.

Umewahi kujiuliza ni kwanini Renard amefanikiwa zaidi Afrika? Ni rahisi tu. Amekuwa kocha anayekutana na timu zenye wachezaji wenye ubora mkubwa na kazi yake kubwa imekuwa ni kuiunganisha tu timu.

Ukirudi nyuma na kukumbuka kikosi cha Zambia chini ya Renard, utakutana na wapiganaji kama Rainford Kalaba, Kennedy Mweene na Chriss Katongo.

Hii haikuwa Zambia ya pole pole. 2015 akishinda Afcon akiwa na Ivory Coast alikuwa na kina Solomon Kalou, Yaya Toure na wapambanaji wengine kibao kutoka Ulaya.

Siri ya kwanza ya kocha kufanya vizuri ni kuwa na wachezaji bora kwanza kisha mbinu zake ndiyo zinapaswa kuanza kuangaliwa.

Mayanga ni kocha mwenye rekodi nzuri kuliko makocha wawili wote waliopita nyuma yake. Kocha Mart Nooij, hakuweza kufikia ubora wa huu aliotufikisha Mayanga. Hata kocha Charles Mkwassa naye hakutufikisha huku.

Kwa kutazama ubora wa wachezaji wetu, tunapaswa kimpongeza sana Mayanga. Baada ya watu kuona Morocco wakifuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, watu wanamuwaza zaidi kocha. Wanashindwa kujua kwamba Morocco waliamua kujipanga kama walivyofanya Misri.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa baada ya Afrika Kusini, basi Morocco ndilo Taifa lingine ambalo limewekeza sana kwenye miundombinu ya michezo.

Renard anaweza kuwa ndiye kocha mwenye mafanikio zaidi barani Afrika lakini ukweli utabaki pale pale.

Akija Tanzania hawezi kutupeleka popote. Bado tunahitaji kuwa watulivu na wavumilivu kufikia ubora wa mataifa mengine.

Tunahitaji kutengeneza wachezaji bora kabla ya kuanza kuwatafuta makocha bora. Matokeo bora hayawezi kujileta yenyewe. Kuna nguvu inahitajika, kuna sadaka itatolewa.

Kwa kutazama uwezo wa wachezaji wetu, Mayanga anatosha kwa sasa. Kwa kutazama aina ya wachezaji tulionao na aina ya matokeo ambayo kocha Mayanga amekuwa akiipatia timu yetu, tunapaswa kujivunia.

Ni kweli bado tuna safari ndefu lakini Mayanga katimiza wajibu wake. Ni kweli tunamhitaji kocha Herve Renard? Hapana, sikubaliani na hilo.

Tunapaswa kutengeneza kwanza ubora wa wachezaji kabla ya kumnyooshea kidole kocha mkuu wa Taifa Stars.

Tunapaswa kuiunga mkono timu yetu ya Taifa na tuna wajibu wa kumuunga mkono kocha wetu pia. Taifa Stars kwanza, mengine yanakuja baadaye.

Tunahitaji kutengeneza wachezaji bora kabla ya kuanza kuwatafuta makocha bora. Matokeo bora hayawezi kujileta yenyewe. Kuna nguvu inahitajika, kuna sadaka itatolewa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.