‘RESPECT’ Mfahamu kipa ‘mhenga’ aliyevunja rekodi ya dunia ya Peter Shilton

Bingwa - - KOLAMU -

LONDON, England

MLINDA mlango aliyedumu mchezoni kwa takribani miaka 29, Paul Bastock anayesakata soka kwenye timu inayoshiriki Ligi Daraja la Tisa nchini England, Wisbech Town, mwishoni mwa wikiendi ilivunja rekodi ya dunia ya kucheza mechi nyingi zaidi kwa ngazi ya klabu (1,250) dhidi ya Thetford Town.

Rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na kipa mkongwe wa zamani, Peter Shilton, ambaye alikuwa na uwezo mkubwa langoni na kumshawishi Bastock mwenye umri wa miaka 47 naye aanze kudaka.

Na juzi dhidi ya timu hiyo katika mchezo wa Kombe Maalumu kwa timu zilizopo chini kabisa, Bastock aliipata nafasi hiyo ya pekee ya kuvunja rekodi ya shujaa wake huyo iliyodumu tangu mwaka 1997, kwa kucheza mechi nyingi zaidi duniani kwa ngazi ya klabu. Kabla ya mechi hiyo, Bastock alizungumzia jinsi anavyolichukulia suala hilo la kuvunja rekodi ya kipa mkongwe aliyewashawishi wengi, si yeye tu, ambapo alisema: “Nilipokuwa mdogo, nilijaribu kuiga kila kitu alichowahi kukifanya Shilton. “Ukiniangalia mwili wangu si mrefu sana, ila nilipenda kubembea kwenye mtambaa panya kuunyoosha mwili kama alivyokuwa akifanya. “Ni kweli walikuwepo Paul Bastock makipa kama vile Ray Clemence, John Burridge na Joe Corrigan, ila Shilton alinishawishi sana niwe kama yeye kila nilipokuwa nikitinga uzi wa njano wa England. Siamini kama nitaivunja rekodi yake.”

Tangu Bastock aanze kucheza soka miongo mitatu iliyopita, ni mengi yamebadilika. Tangu aanze kufanya mazoezi na timu ya vijana ya Coventry City iliyotwaa taji la vijana la FA mwaka 1987.

Hata hivyo, mafanikio hayo hayakumfanya adumu sana Conventry na aliposhindwa kuvumilia kubakia benchi, alitimka akiwa na umri wa miaka 17 na kutua Cambridge United ambako alikutana na jukumu la kumsaidia mlinda mlango namba moja, Keith Branagan.

Lakini, baadaye msimu huo, Branagan alitimkia Bolton Wanderers na Bastock akaanzishwa kikosi cha kwanza katika mechi 10 za mwisho za msimu, akianza mechi yake ya kwanza kwa kutofungwa bao ambapo timu yake ilitoka suluhu dhidi ya Colchester United.

“Naikumbuka vizuri mechi yangu ya kwanza Cambridge. Nilikuwa nina nywele nyingi kiasi na nilivaa viatu vyeusi vya Puma Kings. Mechi iliisha vyema na tulifurahi,” alisema.

Tangu kipindi hicho, Bastock alizidakia klabu 18 zikiwemo zile alizocheza kwa muda mfupi nchini Malaysia (Sabah FA), lakini klabu aliyoitumikia kwa muda mrefu ilikuwa ni Boston United kwa miaka 12 na hadi leo anakumbukwa.

Maisha yake ndani ya klabu hiyo yalitawaliwa na matukio ya furaha, ambapo baada ya kupanda daraja la ‘Football League’, pia aliitwa timu ya taifa ya England ‘C’ baada ya muda wa miaka 10 tu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.