Spesho NOVERTUS KOMBA

MKALI WA TENISI ANAYEWAASA WALEMAVU WENZAKE KUJIKITA KWENYE MICHEZO

Bingwa - - KOLAMU -

NA GLORY MLAY

HAPA duniani kuna watu wameumbwa na Mungu kufanya kazi moja tu, ambayo itamfanya kumudu maisha yake ya kila siku, japo anaweza kufanya kazi nyingine lakini baadaye akajikuta akirejea kwenye ile ile ya awali.

Miongoni mwao ni mchezaji wa tenisi walemavu, Novertus Komba, ambaye anashikilia nafasi ya kwanza ya mchezaji bora katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Komba alianza kucheza tenisi tangu mwaka 2008, akiwa shule ya msingi aliyokuwa akisoma ya Jeshi la Wokovu, Temeke, jijini Dar es Salaam.

Alianza kujifunza mchezo huo hapo shuleni baada ya kupata kocha aliyejitolea kuwafundisha, aliendelea kujifunza mchezo huo mpaka alipohitimu masomo yake ya darasa la saba na kufanikiwa kujiunga na kidato cha kwanza Pugu Sekondari. Akiwa shuleni hapo, aliendelea kucheza tenisi mpaka alipohitimu kidato cha nne mwaka 2012. Komba amefanikiwa kuibuka bingwa kwenye mashindano aliyokuwa akishiriki, yakiwamo ya Kenya Open, Sweden Open, Rwanda Open, BNP Paribas na mengineyo yaliyofanyika katika nchi mbalimbali. BINGWA limefanya mahojiano na Komba ili kujua maisha yake ya sasa na changamoto anazokutana nazo akiwa mchezaji bora wa tenisi kwa walemavu. BINGWA: Uliingia lini rasmi katika mchezo huo wa tenisi? Komba: Nilianza mwaka 2012 baada ya kumaliza kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo kwani sikuweza kuchaguliwa, hapo ndipo niliweza kuitumia nafasi hiyo kuingia kwenye tenisi rasmi. BINGWA: Na mashindano yako ya kwanza kushiriki yalikuwa yapi na ulifanikiwa kushinda au la? Komba: Mashindano yangu ya kwanza kabisa yalikuwa yakiitwa Simba Cement, sikuweza kufanya vizuri kwani ilikuwa mara yangu ya kwanza na yalishirikisha wachezaji kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania. Japo nilifanya vibaya lakini ikiwa ndio mwanzo wa safari yangu ya tenisi kwani niliweza kuchaguliwa na kocha kufundishwa zaidi mchezo huo pamoja na sheria zake.

BINGWA: Mashindano gani ya kwanza ya kimataifa ambayo ulishiriki na kufanikiwa kushinda?

Komba: Mashindano ya kwanza yalikuwa ya Kenya Open na yalikuwa mashindano ya kufuzu kucheza mashindano ya dunia. Yalishirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati, Mungu alinisaidia nilikuwa mshindi wa pili na nilipewa tiketi ya kushiriki mashindano ya dunia pamoja na tuzo ya mchezaji bora mwaka 2013.

BINGWA: Changamoto gani ambazo unakutana nazo katika mchezo huo wa tenisi, pia na kwa wachezaji wenzako?

Komba: Changamoto zipo nyingi, kwanza ukosefu wa viti vya magurudumu (wheelchair), vimekuwa tatizo, unakuta wachezaji tunashea viti, akicheza mchezaji huyo akimaliza inabidi ampe mwenzake aende kucheza, hii ndiyo changamoto kubwa inayoniumiza.

Pili, hatuna programu ya mashindano, hali hii ni changamoto kubwa kwetu, kocha anaweza kuja na kutuambia wiki ijayo mashindano na ukiangalia hatujafanya mazoezi, jambo hili limekuwa likituangusha sana katika mashindano ya kimataifa.

BINGWA: Licha ya changamoto hizo, tumeona unazidi kung’ara katika mashindano mbalimbali ya kimataifa, tuambie siri ya mafanikio yako?

Komba: Unajua mchezo ukiupenda lazima utaucheza kwa moyo, kujituma na kufanya mazoezi kwa bidii ndiyo silaha yangu kubwa ya ushindi.

BINGWA: Mbali na tenisi unajishughulisha na biashara gani?

Komba: Siku ambazo huwa nipo huru nafanya kazi za bajaji, ndio kazi ambayo inaniwezesha kuishi na kufanya mambo mengine, nimepanga na ninaishi peke yangu.

BINGWA: Malengo yako ni yapi katika mchezo huu wa tenisi?

Komba: Malengo yangu ni kufika kumi bora ya wachezaji bora duniani, hiyo ni ndoto ambayo nimejiwekea tangu nilipoupa nafasi mchezo huu katika maisha yangu, ndio maana napambana mchana na usiku kuhakikisha nakuwa bingwa katika mashindano yoyote nitakayocheza.

BINGWA: Ushauri wako ni upi kwa watu wenye ulemavu ambao wanahofia kuingia katika mchezo huo?

Komba: Wajitokeze, mchezo huu bado unahitaji wachezaji, wasiogope kwani siku zote mwanzo huwa mgumu, ulemavu si ugonjwa kwani wanaweza kuingia katika michezo mbalimbali kwani ipo mingi, wajitokeze wasijifiche.

Siku ambazo huwa nipo huru nafanya kazi za bajaji, ndio kazi ambayo inaniwezesha kuishi na kufanya mambo mengine, nimepanga na ninaishi peke yangu.

Mwandishi wa makala haya Glory Mlay akifanya mahojiano na Novertus Komba

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.