NI KAMA MIGUU YAO IMEFUNGWA NATI MSIMU HUU

Bingwa - - JUMATATU SPESHO -

NA ZAINAB IDDY

IMESALIA michezo sita pekee kukamilisha duru la mzunguko wa kwanza la Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuchezwa michezo tisa kwa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo. Katika msimu huu, tayari kila timu imeonekana kukiri kuwa ligi ni ngumu iliyochagizwa na maandalizi mazuri yaliyofanywa kabla ya ligi kuanza, lakini ugumu huo haupo kwa timu shiriki pekee umeonekana kuwakumba hata baadhi ya wachezaji ambao msimu uliopita waling’ara katika uchekaji na nyavu, lakini msimu huu hawaonekani kufanya hivyo jambo linaloonesha wazi miguu yao imefungwa nati. Donald Ngoma Straika wa kimataifa wa Yanga raia wa Zimbabwe, msimu huu unaonekana kutokuwa mzuri kwake baada ya hadi sasa kushindwa kucheka na nyavu.

Kwa sasa Ngoma anasumbuliwa na tatizo la goti, linalomlazimu kuendelea kukaa nje kwa wiki tatu zaidi kabla ya kurejea uwanjani, lakini kabla ya kuanza kukaa nje aliweza kucheza michezo mitano ya ligi ambayo amefanikiwa kuziona nyavu mara mbili pekee na hivyo kuonekana msimu huu kutokuwa na kasi ya ufungaji kama ilivyokuwa msimu uliopita alipoziona nyavu mara tisa. Abdulrahman Mussa Alifanikiwa kung’ara msimu uliopita akichuana vikali na winga wa Yanga, Simon Msuva, anayecheza soka la kulipwa hivi sasa nchini Morocco, katika timu ya Difaa El Jadida, baada ya mchuano wa msimu mzima wa ligi uliopita, Mussa alijikuta akitoka droo na Msuva akifikisha mabao 14 na hivyo wote kupewa tuzo ya ufungaji bora msimu wa 2016/17.

Lakini msimu huu wa ligi miguu yake imeonekana kufungwa nati, kwani hadi sasa akiwa na kikosi chake kile kile cha Ruvu Shooting hajafunga bao lolote kwenye mechi za ligi alizocheza. Wazir Junior Straika anayekipiga katika timu ya Azam FC, msimu huu wa ligi alijiunga nao kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Toto African baada ya kuifanyia kazi kwa vipindi vitatu, akiwa miongoni mwa wachezaji walioipandisha Ligi Kuu msimu wa 2015/16.

Inakumbukwa akiwa na Toto, Waziri alikuwa mwiba kwa timu pinzani kwani kwa misimu miwili tofauti alifanikiwa kuifungia mabao si chini ya nane, lakini msimu huu hadi sasa kikosi chake kipya kikiwa kimecheza mechi tisa hajaweza kuziona nyavu hata mara moja. Rafael Daud Kiungo wa Yanga SC hivi sasa, msimu uliopita alikuwa akikipiga katika kikosi cha Mbeya City ambayo aliweza kuwa miongoni mwa wachezaji walioziona nyavu za wapinzani mara nyingi, kwani akiwa na wagonga nyundo wa Mbeya msimu uliopita, Rafael aliifungia mabao lakini ujio wake Yanga, unaonekana kutokuwa na mafanikio baada ya yale makali yake ya ufungaji kupotea kutokana na kushindwa kuifungia timu yake mpya bao lolote.

Laudit Mavugo

Ni msimu wake wa pili akicheza soka la Tanzania kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Mavugo anayekipiga kwenye kikosi cha Simba aliyojiunga nayo akitokea Vital’O ya Burundi, akiwa mfungaji bora, katika ligi iliyopita aliweza kuisaidia Simba kuifungia mabao nane licha ya kuanza kwa kusuasua, lakini msimu huu hali imekuwa mbaya kwa upande wake baada ya kushindwa kuifungia bao hata moja Simba, licha ya mara kwa mara kupewa nafasi katika kikosi cha kocha, Joseph Omog. John Bocco Ni straika tegemeo katika kikosi cha Simba, waliyemsajili kwa miaka miwili akitokea Azam FC msimu huu, akiwa na Azam kwa misimu kadhaa Bocco alionekana kuwa tishio kwenye nyavu za wapinzani wao na hata kufanikiwa pia kuchukua tuzo ya ufungaji bora msimu wa 2011/12 alipopachika mabao 19, lakini msimu huu ameweza kuziona nyavu mara moja pekee, hivyo kuonekana miguu yake imefungwa nati.

Wakati wanandinga hao miguu yao ikionekana kufungwa nati msimu huu, wapo wachezaji waliofanikiwa kuendeleza makali katika suala zima la kucheka na nyavu kama ilivyokuwa msimu uliopita baada ya kuonekana mara kwa mara wakizipa timu zao mabao.

Wanandinga hao ni pamoja na Shiza Kichuya wa Simba aliyeweza kuziona nyavu mara tano sawa na Ibrahim Ajib wa Yanga, Eliud Ambokile kutoka Mbeya City mwenye mabao manne sawa na Habibu Kiyombo kutoka Mbao FC, wakati Mbaraka Yusuph aliyekuwa Kagera Sugar msimu uliopita hivi sasa ameweza kufunga mabao matatu akiwa na kikosi kipya cha Azam FC.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.