KAMATI YA MAANDALIZI U-17 2019 IFANYE KAZI KAMA MCHWA

Naamini hakutakuwa na longolongo katika kamati hiyo, kwa kuwa inaundwa na watu makini wenye weledi mkubwa katika sekta ya michezo na nyingine.

Bingwa - - UCHAMBUZI/HABARI -

NI habari njema kwa Watanzania kusikia Serikali imeunda kikosi kazi cha maandalizi ya fainali za Afrika kwa vijana waliochini ya miaka 17, zitakazofanyika hapa nchini mwaka 2019.

Kwa Watanzania ni jambo la faraja kuanza kusikia Serikali ikitamka kuwapo kwa mwanzo wa maandalizi ya fainali hizo, ambazo zitapigwa kwa mara ya kwanza hapa nchini.

Pengine nakuwa Mtanzania wa kwanza kuipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuweka mkono katika maandalizi ya fainali hizo.

Ninaamini Watanzania wengine wataendelea kuiunga mkono Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika harakati za kufanikisha fainali za vijana zitakazopigwa miaka miwili ijayo.

Kabla sijaendelea na mada yangu, ningependa kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa kutumia muda wake kuunda kamati ya maandalizi ya fainali hiyo.

Mzee wa Kupasua anaiona kamati ya Waziri Mwakyembe inaundwa na watu makini waliobobea katika sekta ya michezo na nyingine.

Binafsi sina shaka na kamati iliyoundwa na Waziri Mwakyembe, kwani jambo langu ni moja tu kwa kamati kuhakikisha inafanya kazi usiku na mchana kama mchwa ili kufanikisha mahitaji yote kuelekea fainali hiyo.

Kubwa ambalo kamati inatakiwa kuzingatia ni alilosema Waziri Mwakyembe kwamba inatakiwa kufanya kazi mara moja.

Waziri Mwakyembe ameona muda uliobaki katika maandalizi ni mdogo, licha ya kwamba tunaweza kusema unatosha kwa maandalizi, lakini kazi inatakiwa ianze mapema ili kufanikisha mambo yote ya msingi.

Naamini hakutakuwa na longolongo katika kamati hiyo, kwa kuwa inaundwa na watu makini wenye weledi mkubwa katika sekta ya michezo na nyingine.

Mzee wa Kupasua anaamini kamati hiyo itafanikisha maandalizi yote ya fainali hizo kwa kuwa inaundwa na watu ambao ni wazoefu katika sekta mbalimbali.

Lakini katika kamati hiyo, wapo watu wanaotoka Caf na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambao ni Leodgar Tenga na Henry Tandau kutokana na uzoefu wao katika masuala ya mpira watasaidia kutoa mwongozo mzuri kwa kamati iliyoundwa na Waziri Mwakyembe.

Kamati iliyoundwa isiache vilio kwa Watanzania pale itakaposhindwa kufanikisha malengo ya maandalizi ya fainali hizo.

Kwa wajumbe wa kamati hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, mwanasheria Damas Ndumbaro, Dk. Francis Michael na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangalla, hakuna kitu kitakachoharibika.

Wajumbe wengine ni Aboubakar Bakhresa, Yusuph Omary, Ahmed Mgoyi, Khalid Dallah, Nasib Mbaga na Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah.

Wengine ni Dk. Alan Kijazi, Dk. James Dotto ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Kamishna wa Uhamiaji, Dk. Ana Peter, Fred Manoki, Lameck Nyambaya, William Erio, Kelvin Twisa, Ladislaus Matindi na Devota Mdachi.

Naitakia kila la heri kamati hiyo.

Tukutane Jumatatu ijayo

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.