Lipuli FC wataka wachezaji wa mkopo

Bingwa - - UCHAMBUZI/HABARI -

NA TIMA SIKILO

KATIKA kuhakikisha inajenga upya kikosi chake, uongozi wa timu ya Lipuli FC umepanga kuwasilisha maombi yao ya kupata wachezaji kwa mkopo katika timu za Azam FC, Majimaji na Ndanda FC.

Akizungumza na BINGWA jana, kocha msaidizi wa Lipuli, Seleman Matola, alisema katika mechi walizocheza wamegundua timu yao ina mapungufu mengi, hivyo hawana budi kuyafanyia kazi ili waweze kuja na changamoto mpya kwenye mzunguko wa lala salama.

Alisema katika mechi tisa walizocheza, wamegundua wanahitaji wachezaji sita katika nafasi za washambuliaji wawili, viungo wawili, beki wa kati pamoja na beki wa pembeni mmoja ambao wamewaona kwenye timu za Azam FC, Ndanda FC na Majimaji FC.

“Tunafahamu uwezo wa wachezaji wetu, bado tunawaangalia kama kutakuwa na mchezaji ambaye tutaona anafaa tutabaki naye, lakini kwa haraka haraka tunahitaji sita.

“Kwa sasa timu yetu haina fedha, hivyo kusajili kwetu kutatokana na timu nyingine kutusaidia kuwapata kwa mkopo, maana hali ya uchumi ni ngumu tunachofanya ni kuzungumza nao ili tuone watatusaidia vipi.”

Alisema baadhi ya wachezaji wanaowahitaji kwa mkopo tayari wameshazungumza nao, lakini wengine viongozi wa Lipuli wameshabeba jukumu la kuongea na mabosi wake.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.