Hatima kesi ya Lulu kujulikana leo

Bingwa - - BURUDANI -

NA CHRISTOPHER MSEKENA

HUKUMU ya kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili staa wa filamu za Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’, leo inatarajiwa kusomwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa upya, Oktoba 19 iliahirishwa Oktoba 26 mwaka huu baada ya Jaji Sam Rumanyika, kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili yaani upande wa Jamhuri na upande wa utetezi sambamba na maoni ya Wazee wa Baraza.

Uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo ulikuja baada ya Jaji Rumanyika, kusikiliza maoni ya wazee watatu wa baraza ambapo mzee wa kwanza, (Omary Panzi) aliiambia Mahakama kuwa Lulu aliua bila kukusudia, mzee wa pili (Sarah), naye alisema anaweza kusema hakuua kimakusudi na mzee wa tatu (Rajab Mlawa), alisema ameridhika na ushahidi wa pande zote mbili na kwamba Lulu aliua bila kukusudia.

Ikumbukwe kuwa kwa mara ya kwanza Lulu alipandishwa kizimbani Aprili 11, 2012 mbele ya Hakimu mfawidhi wa wakati huo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Augustina Mbando, ambapo alisomewa mashtaka ya mauaji.

Lulu aliachiwa kwa dhamana Januari 29, 2013 baada ya kesi hiyo kubadilishwa hati ya mashtaka kutoka kwenye kesi ya mauaji kwenda mauaji ya bila kukusudia ambapo badiliko hilo lilimpa nafasi ya kupata dhamana, katika kesi ya msingi namba 125 ya mwaka 2012, inadaiwa kuwa Aprili 7, 2012 Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua msanii, Steven Kanumba, bila kukusudia.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.