Stars ililinda heshima kwa Cape Verde, 2008

Bingwa - - MAHABA UNAKUMBUKA -

TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars, ililinda heshima na kukataa kufanywa daraja, baada ya kuilaza mabao 3-1, Cape Verde katika mchezo wa kuwania kutinga fainali za Kombe la Dunia, zilizofanyika mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.

Mchezo huo wa kukamilisha ratiba ya kufuzu fainali hizo, ulichezwa Oktoba 11 mwaka 2008, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Dalili za Stars kushinda zilianza kuonekana mapema baada ya kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Cape Verde, lakini tatizo la umaliziaji liliendelea kuwa ugonjwa sugu.

Kama washambuliaji wa Stars wangekuwa makini katika umaliziaji, wangeweza kupata mabao zaidi waliyoyapata katika mchezo huo, kwani mara kadhaa walikuwa wanalifikia lango la wapinzani wao, lakini mashuti yao mengi yalikuwa yakitoka nje na mengine kudakwa na kipa wa timu ya Cape Verde.

Stars ikishangiliwa na maelfu ya mashabiki walioingia uwanjani kushuhudia mchezo huo, ilipachika wavuni bao la kwanza katika dakika ya sita lililofungwa na kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ ambaye alipokea pasi kutoka kwa kiungo, Nurdin Bakari.

Bao hilo lilizidisha ari ya mashambulizi langoni mwa timu ya Cape Verde na kumfanya beki, Neves Fernand awe kwenye wakati mgumu wa kumdhibiti mshambuliaji wa Stars, Mrisho Ngassa.

Mchezaji ambaye katika mchezo huo alitakiwa kujilaumu mwenyewe alikuwa mshambuliaji Jerry Tegete, baada ya kupoteza nafasi kadhaa za kupachika mabao.

Pamoja na Tegete kupoteza nafasi nyingi za kufunga, lakini dakika ya 27 alifunga bao la pili kwa shuti kali, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ngassa.

Mabao hayo mawili ya Stars yaliwashtua Cape Verde na kuamua kufanya mabadiliko, ambapo walimtoa beki wa kati, Ramos Odysen na nafasi yake kuchukuliwa na Semedo Jase.

Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu na ari kwa Cape Verde, kwani waliweza kupachika bao dakika ya 34 ambalo lilifungwa na Jase.

Licha ya timu zote kuonekana kusaka mabao mengine zaidi, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba na kujikuta dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika kwa Stars wakiongoza kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa Cape Verde kucheza kwa utulivu zaidi kulinganisha na kipindi cha kwanza huku ikipanga mashambulizi kwa lengo la kusaka bao la kusawazisha, mabeki wa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa kushirikiana na Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, walikuwa makini kwa kuondoa hatari zote ambazo zilikuwa zikielekezwa langoni mwao.

Alikuwa ni Ngassa dakika ya 75 aliyeiandikia Stars bao la tatu baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jabu ambaye aliwatoka mabeki wa Cape Verde.

Pamoja na Stars kupoteza matumaini ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika, ilifikisha pointi nane huku Cape Varde ikiwa na pointi tisa.

Stars: Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa ‘Fusso’, Juma Jabu, Salum Sued, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nurdin Bakari, Henry Joseph/ Jabir Aziz, Haruna Moshi ‘Boban’/ Kiggi Makasi, Jerry Tegete/Mussa Hassan ‘Mgosi’, Mrisho Ngassa na Athumani Iddi ‘Chuji’.

Cape Verde: Soarese Erenesto, Monteiro Pedro, Ramos Odyesen/Semedo Jase, Amado Narder/Ramos Heldon, Gomes Eduardo, Agniar Claudio, Marrins Janicio, Soares Marco, Darua Emerson na Valela Fernando.

Kikosi cha Taifa Stars.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.