UONGOZE MOYO WANGU (GUIDE MY HEART) 4

Bingwa - - HADITHI - LIKE PAGE Facebook, za Eman Fisima Hadithi

Ilipoishia Aliendelea kusema kuwa ndege hiyo haijaharibika vibaya ila abiria wengi wamepoteza maisha kwa mujibu wa taarifa ya haraka huku ikidhaniwa kuwa abiria wachache wamepona. Albat aliposikia taarifa hiyo, nguvu zilimuishia alijitahidi kushindana na nguvu ya mwili kwa kutumia akili yake lakini hakuweza. Maumivu makali na ya ghafla yaliushtua moyo wake. Muda mfupi baadaye alidondoka chini na kupoteza fahamu. SASA ENDELEA

Alikuja kuzinduka na kujikuta akiwa hospitalini, alizungusha macho kushoto na kulia asijue nini kilikuwa kikiendelea. Baada ya kujua mahali alipokuwapo, upesi akili yake iliweza kumfahamisha nini kilikuwa kimemtokea mara ya mwisho.

Mapigo ya moyo wake yalianza kumuenda mbio maana alikumbuka kuwa taarifa ya kutokea kwa ajali ya ndege ndiyo iliyomfanya apoteze fahamu.

Albat alijikuta katika hali asiyoielewa, moyo wake ulikuwa tofauti na wa jana, alihisi labda amepata ugonjwa unaokaribiana na ugonjwa wa moyo. Hisia za kichwa chake zilianza kuongozwa na moyo ulioumfanya amkumbuke haraka sana Leo Pordina.

Alijikuta ananyanyuka kitandani na kukaa, muda huo huo aliingia muuguzi wa kike ambaye alionyesha tabasamu pana kwa Albat.

“Umeamka?” aliongea muuguzi huyo huku akiweka baadhi ya vifaa vyake mezani.

Alimfuata Albat aliyekuwa katika hali ya tofauti na siku zote. Si taarifa tu ya ajali ya ndege tu ndiyo iliyomfanya kuwa tofauti, bali alijikuta katika hali mpya iliyomshtua hata yeye mwenyewe.

Alitaka kushuka kwenye kitanda lakini muuguzi alimkataza kufanya hivyo, alijikuta anapinga kulala wala kukaa kitandani, maumivu ya ndani ya moyo wake yaliendelea kumjengea hisia kali zaidi, aliona kama Leo Pordina amekaa kwenye moyo wake na kumletea hali ya tofauti kabisa.

Machozi mengi yalianza kumtoka kiasi cha kumshtua muuguzi, upesi muuguzi alikwenda kumuita daktari. Daktari alifika upesi na kumtazama Albat mara kadhaa.

“Nimeletwa na nani hapa?” aliuliza Albat. “Marafiki zako,” alijibu daktari. “Wako wapi kwa sasa?” “Wako nje tumewataka wasubiri hadi pale utakapoamka.”

“Kuna athari yoyote niliyopata baada ya kupoteza fahamu?” Albat aliuliza.

“Kwanza nataka kujua nini kilitokea nyumbani kwako hadi kupelekea wewe kuanguka?” aliuliza daktari.

“Nakumbuka nilikuwa natazama habari.” “Kuna taarifa mbaya uliisikia?” “Ndio.” “Ni taarifa ipi?” “Ajali ya ndege,” alijibu Albat huku akilengwa na machozi.

“Hata mimi nimeisikia na imenishtua pia je, kuna ndugu yako alikuwa akisafiri na ndege hiyo?” aliuliza daktari. “Ni rafiki yangu.” “Pole sana.” “Je, kuna athari yoyote iliyojitokeza kwenye mwili wangu?” aliuliza Albat.

“Umepata mshtuko mdogo tu nadhani utarudi kwenye hali yako. Ila nakusihi punguza mawazo.”

Baada ya mazungumzo hayo kati ya Albat na daktari, marafiki zake wawili waliruhusiwa kuingia kumwona. Walikuwa ni vijana wa kiume mmoja raia wa Afrika Kusini na mwingine Mtanzania.

“Vipi Albat hali yako ikoje?” aliuliza kijana aitwae Mwita ambaye ni Mtanzania.

“Nzuri tu,” Albat alimjibu kwa hali ya wasiwasi.

“Pole sana tumeshukuru kukuona uko salama maana hali ya mwanzo ilitushtua sana,” aliongea rafiki yake mwingine aitwaye Benard, Mwafrika Kusini.

“Asanteni sana mabesti zangu, lakini nashangaa mliwezaje kufika maana muda ule nilikuwa mimi peke yangu.”

“Sisi tumefika pale saa mbili usiku na ilikuwa kama bahati ya Mungu kwani tulikuwa tumetoka kwa Betty tukaamua tupitie na kwako,” aliongea Mwita.

“Tumekukuta ukiwa chini ukihema kwa mbali sana, yaani kifupi ulikuwa katika hali mbaya.”

“Kwani Albat huwa unaanguka mara kwa mara maana mimi sijawahi kukuona ukianguka?” aliuliza Mwita.

“Hapana ni mara yangu ya kwanza.”

“Ni jambo gani lilipelekea wewe kuanguka? Maana ukiona hadi mtu unapoteza fahamu kunakuwa na jambo lisilo la kawaida,” aliuliza Benard.

“Mi nahisi taarifa ya ajali ya ndege ndiyo iliyokupa mshtuko,” aliongea Mwita.

“Ni kweli Mwita,” alijibu Albat kwa majonzi makubwa.

“Ndiyo imemfanye apoteze fahamu kiasi kile?” aliuliza Benard.

“Hivi Benard hujui kuna wanafunzi wanne wa kutoka Ujerumani walikuwa kwenye ile ndege akiwemo yule msichana kisura Leo Pordina,” aliuliza Mwita.

“Ndio nafahamu kila mwanachuo anaijua hiyo taarifa na tuko kwenye masikitiko makubwa.”

“Sasa bado hujajua kwanini Albat alipoteza fahamu baada ya kusikia taarifa hiyo?”

“Nashangaa Albat kuanguka kabisa mbona hakuna mwanafunzi aliyepoteza fahamu kama yeye ilihali kuwa kila mmoja wetu ameumia kusikia taarifa ile?”

Lakini Benard alikuwa amesahau kuwa Albat na Leo Pordina walikuwa ni marafiki wakubwa. Pamoja na hayo wote hawakujua kama Albat alikuwa kwenye penzi zito juu ya Leo Pordina.

“Tuachane na hayo daktari amekuruhusu kuondoka?” aliuliza Benard. “Ndiyo ila baadaye,” alijibu Albat. Baada ya saa mbili, daktari alikuja kitandani kwa Albat. Alimruhusu Albat kurudi nyumbani lakini Albat alijifikiria mara kadhaa na kuamua kumwomba kitu daktari. Daktari aliwaomba tena Mwita na Benard kutoka nje wakati akiongea na Albat. Baada ya kutoka Albat alimwambia daktari.

“Dk. naomba unifanyie vipimo vya moyo nahisi hali ya tofauti na mwanzo.”

“Nilishakupima kabla hata hujaamka na sijaona matatizo yoyote kwenye moyo wako. Kwani unahisi nini?”

“Nahisi moyo wangu u tofauti kabisa na wa siku zote na hii ni baada ya kusikia taarifa ya ajali ya ndege,” alijibu Albat kwa hofu fulani.

“Mmh inaweza kuwa ni hofu juu ya rafiki yako aliyekuwamo kwenye ndege hiyo. Suala kama hilo kila binadamu anakuwa nalo maana anaumia kwa sababu mtu wake wa karibu anakuwa amepatwa na matatizo au kifo, hivyo usidhani kama kuna jambo lingine tofauti na hilo.” “Hapana nahisi ni zaidi ya hivyo Dk.” “Hebu niambie vizuri ni nani alikuwa mmoja wa abiria kwenye ndege hiyo ni ndugu yako tu?” aliuliza daktari.

“Ukweli ni kwamba ni msichana ninayempenda sana.”

“Sasa Albat hilo suala liko kimapenzi zaidi, wewe unateseka kwa sababu aliyepata ajali ni msichana unayempenda hivyo lazima moyo wako ujenge hofu ya kimapenzi.”

“Pamoja na hayo, Dk nahisi moyo wangu uko zaidi ya hivyo.” “Kivipi hebu nieleze vizuri Albat.” “Wakati niko karibu na msichana yule sikuwa katika hali hii ingawa nilikuwa kwenye mateso makubwa ya kimapenzi. Lakini kwa sasa ni zaidi ya hivyo, maumivu yake yamekuwa zaidi ya mwanzo nahisi kuna nafsi yake inaushikilia moyo wangu maana kuna muda nahisi moyo wangu ni mzito sana.”

Daktari alizidi kutoelewa vizuri maelezo ya Albat, alianza kuhisi kuwa huenda Albat anakwenda kuchanganyikiwa.

“Albat binafsi nimekuelewa kwa namna ninavyofahamu mimi kuhusu mapenzi na hofu ya kumpoteza mtu umpendaye na si vinginevyo. Ila nakushauri nenda kwa mtaalamu wa saikolojia huenda tatizo la moyo wako linaweza kuwa linaunganishwa na hali fulani ya kisaikolojia,” aliongea daktari huku akisimama kwenye kiti kilichokuwa karibu na kitanda.

Albat hakuwa na namna nyingine, hali hiyo iliyokuwa ikimsumbua moyoni mwake, alihifadhi kama maumivu yake ambayo yanamhitaji yeye mwenyewe kuyatatua.

Baadaye aliruhusiwa kurudi nyumbani. Aliondoka yeye na marafiki zake, ambao walimsindikiza hadi nyumbani kwake. Wakiwa wamekaa huku wakipata vinywaji. Benard aliwasha runinga, habari kutoka kituo cha televisheni cha E tv ilikuwa ikitangazwa.

Wote walikaa sawa baada ya kukuta taarifa iiliyowahusu, bado vyombo vya habari duniani kote viliendelea kuhabarisha kuhusu ajali ya ndege iliyotokea jana mchana.

Taarifa hiyo ilisema kuwa katika uchunguzi wa mwisho wa ajali hiyo ni abiria sita tu kati ya abiria 150 waliopona. Na wamepelekwa hospitali isiyo na huduma kubwa na jeshi la Serikali lililokuwa maeneo ya karibu.

“Mungu wangu sidhani kama wale wanafunzi wa Kijerumani wamepona,” aliongea Benard.

“Hapo ni ngumu sana abiria 150 wote wamepoteza maisha,” aliongezea Mwita.

“Yule binti mzuri Leo Pordina daah! Inaniuma sana,” aliongea Benard. Albat akiwa katika hali ya majonzi yasiyoelezeka, alikuwa amekaa kimya wakati wenzake wakiongea, machozi mengi yalianza kumtoka, alijikaza kiume lakini alishindwa, upesi aliinuka na kuelekea chumbani kwake ambako alijitupa kitandani na kulia sana. Alihisi maumivu makali moyoni, ambayo hakuwahi kuyasikia tokea azaliwe.

Benard na Mwita walishtuka kuona rafiki yao ameondoka haraka pale sebuleni, Benard alimwita Albat. “Albat!!!” “Hapana Benard usimwite mwache,” Mwita alimkataza. “Why?” (kwanini?) “Ina maana hujui ajali hii jinsi inavyomuumiza, hujui Leo Pordina alikuwa rafiki yake?” aliuliza Mwita.

Huko chumbani kilio kikubwa kiliendelea kwa Albat, alishindwa kujizuia maana alimpenda sana Leo Pordina. Hakutaka kuamini kama msichana mzuri kama yule afe kirahisi namna ile, tena akiwa amemwachia ahadi ya kumpa jibu lake pindi atakapofika Ujerumani. Hakika naye alitamani kufa ili amfuate huko aliko.

Nini kitafuatia? Usikose kesho.

Daktari alizidi kutoelewa vizuri maelezo ya Albat, alianza kuhisi kuwa huenda Albat anakwenda kuchanganyikiwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.