DONALD NGOMA AKIONA CHA MOTO YANGA

Bingwa - - MBELE -

ZAINAB IDDY NA HUSSEN OMAR

AMA kwa hakika Yanga hatawaki kupandwa kichwani na mchezaji, hilo likiwa limejidhihirisha kutokana na uamuzi wao wa kumkata mshahara straika wao wa kimataifa, Donald Ngoma kutokana na tuhuma za utoro.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani zilizopatikana kutoka Yanga jana, zinasema kuwa Mzimbabwe huyo anakatwa kiasi cha Dola za Marekani 100 sawa na Sh 219,730 kwa kila siku aliyokuwa nje ya kikosi.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya klabu hiyo kuchoshwa na tabia ya Ngoma kuwaendesha viongozi wa Yanga kwa kufanya vile anavyotaka.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, aliliambia BINGWA jana kwamba, Ngoma amekuwa akionyesha utovu wa nidhamu kwa kuchukua maamuzi ya kuwa nje na timu, huku benchi la ufundi wala uongozi wa juu wakiwa hawana taarifa yoyote.

“Umefika wakati wa kunyooshana, maana hivi sasa Ngoma ameonekana kutaka kutupanda kichwani kwani hii ni mara ya pili kama si ya tatu anaondoka nchini au anakacha mazoezi bila ya kutoa taarifa yoyote na anaporudi anaomba msamaha tu, kisha tunamwachia.

“Kitu tulichogundua Ngoma amechoka maisha ya ndani ya Yanga, anapaswa kusema kwani hatumlazimishi mchezaji yeyote kufanya kazi kwetu, lakini suala la kuondoka na kurudi vile anavyotaka, limefika mwisho, tulichokiamua ni kumkata Dola 100 kwa kila siku ambayo hakuwepo na timu,” alisema.

Alisema fedha anazokatwa Ngoma ni zile za mshahara wake wa Oktoba, hivyo kadiri siku zinavyozidi kwenda, mshahara wake utakuwa ukipungua.”

Kwa kuwa Ngoma aliondoka Tanzania kwenda Zimbambwe Oktoba 22, mwaka huu, wakati Yanga ikicheza mechi dhidi ya Stand United, Wanajangwani wakishinda mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, hadi jana ameshatimiza siku 21 hivyo atakatwa Dola 100 za Marekani 2100, sawa na Sh milioni 4.6.

Wakati Ngoma akikutwa na kisanga hicho, wachezaji wenzake wanatarajiwa kuonja ladha ya mshahara baada ya uongozi wa timu hiyo kuwaahidi kuwalipa mishahara ya miezi miwili kila mmoja kabla ya mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakaochezwa mwishoni mwa wiki hii.

Wachezaji wa Yanga wamekuwa wakiishi maisha magumu kwa miezi minne sasa kutokana na kutolipwa mishahara, huku wakiendesha maisha yao kwa kutumia posho pekee pamoja na motisha kutoka kwa wahisani, hasa pindi timu

inapofanya vizuri.

Wakizungumza na BINGWA kwa nyakati tofauti, wachezaji wa timu hiyo walisema walikutana na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa na kuzungumza naye ndipo alipowapa habari njema ya kupewa mishahara yao kabla ya kwenda mapumzikoni.

“Katibu alituambia kabla ya mechi yetu na Mbeya City tutakuwa tumeshalipwa miezi miwili, huku nyingine zilizobaki tutamaliziwa tukiwa likizo kwani haipendezi tunarejea majumbani kwetu mifukoni hatuna kitu,” alisema.

Kuhusu fedha za kusaini mikataba wanayodai wachezaji hao, walisema wamewahakikishia watalipwa kabla ya usajili wa dirisha dogo.

“Katibu ametuambia tayari ameshaongea na viongozi wenzake wasifanye usajili mpya ikiwa hawajakamilisha madeni ya wale wa zamani, hivyo bila shaka siku si nyingi mifuko yetu itanenepa,” alisema mchezaji mwingine.

BINGWA lilipomtafuta Mkwasa kujua ukweli juu wa hayo, alikiri kuwapo kwa wachezaji wanaodai na kusema ni jambo la kawaida kwa kuwa si Yanga pekee inayodaiwa misharaha na wachezaji wake katika soka la Tanzania.

“Si jambo geni Yanga kudaiwa, zipo timu nyingi tu na niseme tu hili suala muda si mrefu litamalizika kwani tupo kwenye mchakato ili kila mchezaji anayedai apewe haki yake,” alisema Mkwasa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.