SIMBA WAIFANYIA UMAFIA YANGA

Bingwa - - MBELE -

ZAINAB IDDY NA WINFRIDA MTOI

SIMBA wavurugaji bwana! Ndivyo unavyoweza kusema kwani baaada ya kusikia watani wao wa jadi, Yanga, wapo katika harakati za kumnasa mshambuliaji wa Mbao FC, Habibu Kiyombo, nao wamepita mlango wa nyuma na kuanza mazungumzo naye.

Yanga walianza kuifuatilia saini ya Kiyombo kabla ya kuanza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, lakini walishindwa kumpata baada ya mchezaji mwenyewe kuhitaji kupewa muda kufikiria hilo.

Kuelekea kwenye dirisha dogo la usajili linalofunguliwa keshokutwa, tayari Yanga wametupa karata yao tena wakiwa na matumaini ya kumpata, lakini wakiwa wanasubiri, Simba nao wamepiga hodi kwa mchezaji huyo.

Akizungumza na BINGWA jana, Kiyombo alisema suala la kuhitajika na timu hizo za Kariakoo analifahamu tangu mwanzoni mwa msimu, hivyo kurejea tena kwao kwake si kitu kigeni.

“Yanga walianza kunifuata kabla ligi haijaanza na tukakaa mezani kuzungumza nikiwapa mahitaji yangu nao kunipa mikakati yao, lakini nilishindwa kusaini baada ya kutokuwa tayari kuondoka Mbao kwa maana ya kutaka kukua zaidi kisoka.

“Kwa siku za hivi karibuni nimekuwa nikipokea simu kutoka kwa viongozi wa Simba wakinieleza wazi nia yao kipindi ambacho tayari Yanga wameshakuja kwa mara ya pili kunihitaji, lakini wote nimewaambia wasubiri kwanza hadi pale nitakapokutana na wale walionikuza kisoka na kuongea

nao,” alisema.

Alisema kuhusu mkataba wake na Mbao, hauna tatizo kwani hata mara ya kwanza alipokuwa anao wa miaka miwili, mabosi wa timu yake walikuwa tayari kumruhusu.

“Viongozi wangu wa Mbao hawana tatizo, kikubwa wapewe taarifa mapema kwa kufuata taratibu za kimkataba,” alisema.

Wakati huo huo, Wekundu wa Msimbazi hao wametua kwa kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohamed Issa ‘Mo Banka’, kutaka kuharibu dili lingine la Yanga kwa kumtangazia dau nono mchezaji huyo.

Habari za ndani ilizozipata BINGWA ni kwamba baada ya Simba kusikia mchezaji huyo anafukuziwa na watani wao hao, wameamua kuingilia kati wakitamba wao ndio wanaweza kumnunua kiungo huyo kutokana na ukaribu wao na Mtibwa Sugar.

Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, alikiri kusikia taarifa za wachezaji wake kadhaa kufukuziwa na timu hizo mbili za Dar es Salaam na kusema anayehitaji mchezaji, aonane na uongozi kuliko kuzungumzia pembeni.

“Taarifa zote za usajili zinapitia kwa uongozi na hizo za kina Mohamed Issa nazisikia tu, hadi sasa sina uhakika, sisi hatuna shida pale mchezaji atakapoona kuna masilahi aende,” alisema Katwila.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.