Stars yaibana Benin ikibebwa kwao

Bingwa - - HABARI -

NA MWANDISHI WETU, BENIN

PAMOJA na kupewa penalti isiyostahili, Benin imeshindwa kutoka uwanjani na pointi zote tatu baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ukiwa ni mchezo wa kirafiki uliopo kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Benin ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 30 kupitia kwa nahodha wake, Stephane Sessegnon, aliyeuweka kimiani mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi wa mchezo huo kwa madai ya mchezaji wa Stars kuunawa mpira wakati haikuwa hivyo.

Marudio ya mchezo huo uliokuwa ukionyeshwa ‘live’ na Azam TV, yaliyonyesha kuwa alikuwa ni mchezaji wa Benin aliyeunawa mpira, tena ikiwa ni nje ya 18 na si wa Stars.

Pamoja na kufungwa bao hilo, wachezaji wa Stars walitulia na hatimaye kusawazisha kupitia kwa Elias Maguli na kufanya timu hizo kutoshana nguvu kwa sare hiyo ya 1-1.

Maguli alifunga bao hilo dakika ya 50 baada ya kupokea krosi murua iliyochongwa na Shiza Kichuya kutoka wingi ya kushoto.

Kwa ujumla mchezo huo ulikuwa mkali kwa muda wote ambapo pamoja na wenyeji kucheza kwa nguvu mno, walijikuta wakitulizwa na vijana wa Stars chini ya unahodha wa Himid Mao.

Stars walipata nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini hazikuzaa matunda, ikiwamo ya dakika 48 pale Simon Msuva alipotoa pasi safi kwa Magulia ambaye alishindwa kuifikia na mpira ukatoka nje.

Kikosi cha Stars: Aishi Mnaula, Himid Mao, Gadiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondani, Mudathir Yahaya/Nurdini Chona dk90, Simon Msuva, Rafael Daudi/ Mbaraka Yusuf dk55, Elias Maguli, Hamis Abdalah/ Jonas Mkude dk75 na Shiza Kichuya/ Ibrahim Ajib dk65.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.