JKT, OILERS WALIVYOSHINDWA KUTUMIA UWANJA WA NYUMBANI

Bingwa - - EXTRA - NA GLORY MLAY

MARA nyingi Tanzania imekuwa ikiandaa michuano ya Klabu Bingwa Kanda ya Tano ‘Zone 5’, lakini imekuwa ikiambulia patupu kutokana na kushindwa kutumia vizuri viwanja vya nyumbani.

Ni mara ya sita sasa michuano hiyo inaandaliwa hapa nchini, lakini timu za Tanzania zimekuwa zikitolewa mapema kutokana na sababu mbalimbali.

Michuano ya mwaka huu iliyomalizika wiki iliyopita Uwanja wa Ndani wa Taifa, ilishirikisha timu kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Kenya, Uganda, Rwanda, Misri, Sudan Kusini, Ethiopia na wenyeji Tanzania.

Katika michuano hiyo, timu ya wanaume ya Al-Alhy ya Misri na ya wanawake Equity ya Kenya, ndio walikuwa mabingwa wa Zone 5 kwa mwaka huu ikiwatupilia mbali wenyeji wao.

Timu za Misri na Kenya zimeendelea kutawala katika michuano hiyo kwa kutwaa ubingwa mara kwa mara huku wenyeji tukiangukia pua.

Wadau na mashabiki wengi walitegemea ushindani uliokuwepo katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) ungeenda moja kwa moja Zone 5, lakini ilikuwa tofauti kwani hawakuweza kufua dafu.

BINGWA lilipata nafasi ya kufanya mazungumzo na makocha, viongozi wa TBF kuhusiana na changomoto za kushindwa kufanya vizuri kwenye Zone 5.

Sababu za Tanzania kushindwa Zone 5

Phares Magesa ambaye ni Rais wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), anasema udhamini umekuwa changamoto na kusababisha timu kushindwa kufanya vyema kwenye michuano ya Zone 5.

Anasema kukosekana kwa wadhamini timu zinashindwa kufanya maandalizi ya kutosha na matokeo yake kuboronga kwenye michuno hiyo.

“Timu zilijitahidi mpaka pale zilipofika na zilionyesha ushindani mkubwa, lakini bado tunachangamoto ya udhamini, timu nyingi zinashindwa kujiandaa ipasavyo kutokana na hazina fedha za kutosha, naamini wangepata wadhamini wangefanya makubwa,” anasema.

Frankiln Simkoko Ni kocha wa timu za JKT wanawake na wanaume, anasema sababu ya kwanza ya kupoteza michezo yao ilitokana na wachezaji wake kuishiwa pumzi.

Simkoko alisema sababu hiyo iliwafanya wachezaji wake kushindwa kuhimili mikikimikiki ya wapinzani wao.

“Wachezaji wetu hawana pumzi kabisa, wakati wenzetu wana uwezo wa kucheza dakika zote,” anasema Simkoko.

Alisema pamoja na tatizo la pumzi, lakini walikosa umakini, kujisahau na kupoteza mipira.

Simkoko alisema mara kwa mara amekuwa akiwaeleza wachezaji wake mchezo wa kikapu unahitaji akili nyingi na mbinu za kumtoka adui.

Simkoko alisema sababu nyingine, wachezaji wake ni wafupi wakilinganishwa na wapinzani wao ambao wana miili mikubwa iliyopanda juu.

Baraka Sadiki Ni mchezaji wa timu ya JKT anasema kuwa hawakuwa na maandalizi ya kutosha kuelekea kwenye michuano hiyo ya Zone 5.

Anasema pia uchovu waliokuwa nao baada ya kutoka kwenye Ligi ya RBA nao ulichangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kufanya vizuri.

“Tulimaliza ligi ya RBA hatukupumzika kwahiyo ule uchovu tuliokuwa nao ndio tuliingia nao Zone 5 ndio maana tulishindwa kufanya vizuri, ushindani ulikuwepo na tulijitahidi kwa uwezo wetu tuliokuwa nao na tukafika

tilipofika,” anasema.

Lusekolo Mbwele Ni kocha wa timu ya Oiler ambayo ilifanikiwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo, alisema hatua waliyofikia ni kubwa ukilinganisha na ushindani uliokuwepo.

Anasema walicheza kadiri ya uwezo wao japo wengine walikuwa majeruhi, lakini walipambana hadi kuingia robo fainali ila hawakuweza kufika mbali.

Mabingwa wazungumzia ushindi wao Kocha wa timu ya wanawake ya Kenya Equity ambao ni mabingwa wa Zone 5 msimu huu, Cavey Odhiambo, alisema maandalizi mazuri waliyofanya ndiyo yaliyowapa ubingwa huo.

Anasema walianza maandalizi Agosti mwaka huu na lengo lao kubwa ni kunyakua ubingwa na hawataangalia ushindani utakaokuwepo kwenye michuano hiyo.

“Tulijipanga kuhakikisha tunachukua ubingwa kwa msimu huu, tulianza maandalizi mapema na tulijiwekea malengo na tunamshukuru Mungu yalitimia,” anasema.

Anasema changamoto kubwa waliyokutana nayo katika michuano hiyo ni usafiri ambao ulikuwa ukiwachukua kutoka uwanjani kwenda hotelini.

Anasema mara nyingi ulikuwa ukichelewa na kusababisha wao kushindwa kufika uwanjani kwa wakati uliopangwa.

Quinton Doggett Aliibuka mchezaji bora wa timu ya Al- Ahly ya Misri, anasema wao huwa wanafanya maandalizi ya muda mrefu ndio maana wamekuwa wakishinda katika michuano hiyo.

Anasema timu nyingi wanajua uchezaji wao hivyo hujifunza mbinu nyingi zaidi ambazo wanaona zitawapa mafanikio zaidi.

“Tunashukuru tumechukua ubingwa kutokana na maandalizi mazuri tuliyofanya, michuano kama hii huwezi kucheza kwa mazoea lazima mjitume na mlete kitu kipya ambacho wapinzani wenu hawawezi kuwaiga au kuwashinda.

“Ushindi unatokana na ubunifu wa wachezaji, mkiwa wabunifu mnapata ushindi ambao hawa watu wengine hawataweza kutegemea hili,” anasema Doggett.

Mikakati ya TBF Phares Magesa alisema nguvu kubwa sasa wataihamishia katika timu hizo ili ziweze kufanya maandalizi ya kutosha.

Alisema pia wanasaka wadhamini wa kudumu ambao wataziwezesha timu hizo kwa kila hali ili kuipa sifa Tanzania kupitia mchezo huo.

“Michuano ipo mingi hivyo tunahitaji kuwekeza nguvu kubwa katika timu zetu ili ziweze kufanya maandalizi ya kutosha, tunasaka wadhamini wa kudumu ili waweze kukidhi mahitaji ya timu hizo.

“Pia kabla ya mashindano tutakuwa tunaweka programu za maandalizi ya muda mrefu ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa fiti kukabiliana na ushindani utakaokuwepo kwenye michuano hiyo ya kitaifa na kimataifa,” anasema.

Wadau na mashabiki wengi walitegemea ushindani uliokuwepo katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (RBA)

Kenya Equity

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.