TAHARUKI KUTEKWA MO DEWJI

Nchi yatikisika, Try Again atoa neno

Bingwa - - MBELE - NA ZAITUNI KIBWANA

WAKAZI wa Jiji la Dar es Salaam, Tanzania na Afrika, wamepatwa na taharuki kutokana na kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini ambaye pia ni mwanachama na mwekezaji ndani ya Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’.

Mfanyabiashara huyo, alitekwa jana asubuhi wakati akielekea katika klabu ya mazoezi (gym) ya Colosseum, jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana.

Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa Mo alitekwa saa 11 alfajiri mara alipoingia katika gym hiyo.

Mambosasa alisema: “Mohammed Dewji maarufu kwa jina la Mo, ametekwa leo (jana), alikuja (katika gym hiyo) kwa ajili ya kufanya mazoezi saa 11 alfajiri, alipofika kulikuwa na gari moja lililotangulia kabla yake, lilipaki kwa mbele, lakini kulikuwa na gari lingine lililokuwa limesimama nje.

“Gari lililokuwa ndani, liliashiria kwa kuwasha taa baada ya Mohammed kuingia. Kwa hiyo gari lililokuwa nje likaingia ndani na kwenda kupaki karibu na gari la Dewji.

“Dewji alipotoka, walitoka wazungu wawili na kumbana Dewji na kumwingiza kwenye gari lao na kuondoka naye.”

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kuwataka Watanzania kutoa ushirikiano juu ya tukio hilo.

Alisema wanawashikilia watu watatu ambao wanahusishwa na tukio hilo la kusikitisha, ambapo aliahidi kuyaweka wazi majina yao hapo baadaye.

Kwa kiasi kikubwa tukio hilo limetikisa mno na kuwagusa wengi, kuanzia wapenzi wa Simba na wa timu nyingine, lakini pia ndugu, jamaa, marafiki wa mfanyabiashara huyo na Watanzania kwa ujumla.

Si hapa nchini pekee, hata nje ya Tanzania, habari za kutekwa kwa Mo Dewji zimewagusa wengi, wakiwamo raia wa ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hata Watanzania waishio ughaibuni, wakionekana kushangazwa na jinsi tukio hilo lilivyotekelezwa.

Ni kutokana na hilo, BINGWA limewasiliana na wadau mbalimbali wa michezo, hasa soka kupata maoni yao juu ya tukio hilo la kusikitisha. Wanachama Simba wapagawa Wanachama wa Simba wakiongozwa na mwanachama mwenye kadi namba 00547 kutoka Tawi la Mpira Pesa, Said Mohamed ‘Bedui’, amepinga vikali tukio hilo.

“Haya si matukio mazuri kwa taifa letu, sio Mo, hata mimi tukio kama hili likinitokea sio zuri ila tunawaachia Jeshi la Polisi wafanye kazi yao,” alisema.

SIMBA WAVUNJA MAZOEZI, WACHEZAJI WANENA

Kwa upande wa ndani ya klabu ya Simba, kutekwa kwa Mo kumeonekana kuwa pigo kubwa kwao kitendo kilichoulazimu uongozi kuvunja mazoezi ya timu hiyo yaliyopangwa kuendelea jana jioni kwenye Uwanja wa Boko Veterans, kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Stand United.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa Simba, Abbas Ally, alisema wameamua kusitisha mazoezi kutokana na majanga hayo ya bilionea wao.

“Tutakuwa watu wa ajabu sana kama tukifanya mazoezi leo (jana), tumeamua kusitisha mazoezi kwa siku yote kwanza kutokana na majanga haya,” alisema Abbas.

Wakati Abbas akiyasema hayo, kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula, alimwomba Mungu amfanyie wepesi bilionea huyo aweze kuwa huru.

“Ewe Mola wetu, mfanyie wepesi kwenye mapito na mtihani alioupata, mfanye awe mwenye kuyashinda mapito hayo na kuwa huru,” aliomba Manula.

Kwa upande wake, kipa Said Mohamed ‘Nduda’, alisema tukio hilo limemshtua na hakutarajia kulisikia masikioni mwake, ila anamwomba Mungu, bilionea huyo apatikane salama.

“Kwa kweli nilikuwa nimelala, nakuja kuwasha simu nakutana na habari za kutekwa, nilishtuka sana, si tukio zuri na nimesikitika sana ila namwombea Mungu aweze kupatikana salama,” alisema.

Naye beki wa timu hiyo, Shomary Kapombe, ambaye kwa sasa yupo timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inayojiandaa na mechi ya kutafuta tiketi ya kufuzu Afcon dhidi ya Cape Verde, aliomba Mo apatikane salama.

“Eeh Mungu, nenda kamtie nguvu na kumlipa na awe katika ushindi kwenye hili, tunakuombea kwa Mungu,” alisema. Uongozi Simba watoa tamko Uongozi wa Simba kupitia Ofisa Habari wake, Haji Manara, waliomba wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi linaendelea na majukumu yake.

“Tunawaomba sana Wanasimba na Watanzania wote tuendelee kuwa watulivu, tujiepushe na uzushi wowote wa mitandaoni, jukumu la utoaji taarifa za kupatikana au la, tuwaachie polisi, sisi tuendelee kuongeza dua na sala ili kiongozi wetu apatikane akiwa mzima na salama,” alisisitiza Manara.

Kwa upande wake, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, amewataka mashabiki wa timu hiyo kutulia na kuomba dua.

“Ni tukio la kusikitisha na Watanzania hususan wanachama wa Simba watulie, jambo linalotakiwa kufanywa sasa ni kumwombea dua, ili mwenzetu awe salama huko alipo,” alisema Try Again akiwa Cape Verde.

YANGA, COASTAL WASHTUSHWA Klabu ya Yanga na Coastal Union 'Wagosi wa Kaya', wameungana na Watanzania kupinga tukio hilo la kutekwa bilionea huyo namba moja kijana barani Afrika. Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten, alisema: “Kitendo hiki ni cha kusikitisha sana, ukiangalia mtu kama Mo analeta maendeleo katika soka, hivyo kila mtu ameumia, tunamwombea kwa Mungu aweze kupatikana akiwa salama na kurejea katika shughuli zake za kila siku,” alisema Ten. Ofisa Habari wa Coastal Union, Hafidhi Kido, alisema wameshtushwa na tukio hilo aliloliita la aibu. “Hili ni tukio la aibu, tunaungana na Watanzania kumwombea mdau huyu wa soka, huko alipo awe salama, tunatumai kwa sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake vizuri ili ndugu yetu apatikane akiwa salama, arudi kwenye shughuli za kujenga nchi, Coastal Union, tupo bega kwa bega na familia ya Mohammed Dewji, katika kipindi hiki kigumu cha majaribu,” alisema. Naye Ofisa Habari wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alisema tukio hilo linapaswa kukemewa kwa nguvu zote, kwani halileti sifa nzuri kwa taifa kwa sasa. “Tunatakiwa kumwombea Mo, apatikane akiwa salama lakini haya matukio yanapaswa kukemewa na hayapendezi kwenye jamii,” alisema. Naye Mwenyekiti wa Alliance FC, James Bwire, aliomba wananchi kutulia na kuliachia suala hilo Jeshi la Polisi kwa kuwa ndio mwenye haki ya kulizungumzia. “Hili suala Jeshi la Polisi ndio wanapaswa kulizungumzia ila tunamwombea, sio yeye tu mtu yeyote akitekwa sio tukio zuri kabisa,” alisema.

MO DEWJI NI NANI

Mohammed Dewji ‘Mo’ alizaliwa Mei 8 mwaka 1975 katika Kata ya Ipembe, mkoani Singida, akiwa ni mtoto wa pili wa Mzee Gulam Dewji kati ya watoto sita wa familia hiyo.

Mfanyabiashara huyo ana dada mmoja aitwaye Sabera na wadogo zake wanne wanaofahamika kwa majina ya Ali, Hassan, Hussein na Fatema.

Mo alipata elimu ya msingi katika Shule ya Arusha na kuhitimu mwaka 1986, kabla ya mwaka 1987 kujiunga na Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST).

Alimaliza elimu yake ya sekondari mwaka 1992 na huo kuwa mwisho wake wa kusoma hapa nchini Tanzania.

Mwaka 1992 alikwenda kuongeza elimu yake nje ya nchi, katika Shule ya SaddleBrooke High School ya Marekani.

Alipomaliza elimu yake hapo Saddle Brooke, Mo alipata nafasi ya kujiunga na Chuo Kikuu cha GeorgeTown cha jijini Washington D.C, Marekani alikosomea mambo ya biashara ya kimataifa na fedha, huku akichukua Theolojia kama somo la ziada.

Alipohitimu masomo mwaka 1998, Mo alirejea nyumbani Tanzania na moja kwa moja akaingia katika biashara za baba yake, Mzee Gulam na akaanza na nafasi ya Mdhibiti Mkuu wa Fedha katika Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (METL).

Mwaka 2001, Mo aliacha ukapera na kuamua kumuoa Saira, ambaye wamejaliwa kupata watoto wawili, mmoja wa kike aitwaye Naila na wa kiume, Abbas.

SIMBA NDIO BOSI WAO

Mo alianza kuwa mfadhili Simba mwaka 2002, ambapo mwaka 2003 aliiwezesha timu hiyo kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwatoa Zamalek ya Misri.

Bilionea huyo kijana Afrika, Desemba 3, mwaka 2017, alitangazwa rasmi kuwa mshindi wa zabuni ya asilimia 50 kuwekeza ndani ya klabu hiyo kwa thamani ya Sh bilioni 20.

Mo pekee ndiye aliweka dau la Sh bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu hiyo kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh bilioni 20, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.

Lakini mfanyabiashara huyo, alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu hiyo kulingana na maelekezo ya Serikali.

Toka alipokabidhiwa timu hiyo, Simba imekuwa ikifaidika na ufadhili wake hasa baada ya kutimiza ahadi zake nyingi, likiwamo suala zima la ujenzi wa uwanja wa kisasa ambao tayari ameanza kuujenga na unatarajia kukamilika Februari mwakani.

Mbali na uwanja huo, Mo aliwezesha usajili kufuru kwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu ili kuifanya timu hiyo kuwa tishio si tu Tanzania, bali pia Afrika.

Si Simba tu, Mo pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde mwaka 2013 iliyowahi kuundwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ikiwa na wajumbe wengine kama Ramadhani Dau, Zitto Kabwe, Teddy Mapunda na Dioniz Malinzi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.