TEMBEA NA MECHI HIZI

Bingwa - - IJUMAA SPESHO -

NI kipindi kingine cha mechi za kimataifa, kuanzia michuano ya Ligi ya Mataifa Ulaya hadi zile za kirafiki, tunaendelea kukupa dondoo motomoto za ubashiri.

CROATIA V ENGLAND Baada ya kupita miezi mitatu, timu hizo zitakutana tena leo, huku England wakiwa na lengo la kulipiza kisasi kwa Croatia, ambao waliwatoa katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Urusi mwaka huu. Croatia, ambayo haijafungwa nyumbani katika mechi12, itaikaribisha England, ambayo haijapoteza mechi 19 za ugenini.

Safari hii wanachuana kwenye Ligi ya Mataifa Ulaya, ingawa hawapo katika nafasi nzuri sana katika msimamo baada ya kupoteza mechi za ufunguzi na njia nzuri ya kupata pesa katika mchezo huo ni kubashiri timu zote zifungane kutokana na uwezo wao wa kufanya mashambulizi.

Utabiri: Croatia 1-1 England

UBELGIJI V USWISI Baada ya kufanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, Ubelgiji wanategemewa kuendeleza kiwango chao bora dhidi ya Uswisi. Ni moja ya mechi kali za Ligi ya Mataifa Ulaya wiki hii, hasa ikizingatiwa vikosi hivyo vilishinda mechi zao za ufunguzi.

Wenyeji wa mchezo huo wana rekodi nzuri zaidi ya kufunga angalau mabao mawili katika mechi sita za mwisho, hivyo Uswisi ambao wamepoteza mechi mbili za mwisho walizocheza ugenini, watakuwa na kazi ya ziada kuwazuia akina Eden Hazard.

Utabiri: Ubelgiji 4-0 Uswisi

MAREKANI V COLOMBIA Wababe hao wa Bara la Amerika watachuana leo pale jijini Florida, huku wageni, Colombia wakionekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo dhidi ya wenyeji wao ambao ndio wanasuka kikosi chao chenye vijana.

Kwa ‘odds’ zilizopo ukijumlisha na rekodi ya mechi walizoshinda Colombia hadi sasa, wageni hao ndio wa uhakika zaidi. Wameshakutana na Marekani mara mbili kwenye Copa Amerika 2016 na ya 2014, na zote waliibuka washindi.

Utabiri: Marekani 0-2 Colombia

UHOLANZI V UJERUMANI Mahasimu hao wa zamani watakutana kesho katika mchezo wa Ligi ya Mataifa Ulaya, timu zote zikisaka ushindi wao wa kwanza katika mashindano hayo na inatarajiwa kuwa mechi kali baina ya miamba hao.

Kwa kiasi kikubwa Uholanzi ndio watakaopata tabu kesho, kwa kuzingatia matokeo ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ufaransa, ambao walishindwa kuhimili mikiki mikiki yao.

Utabiri: Uholanzi 1-2 Ujerumani

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.