KOSA KUBWA WANALOFANYA WANAUME KWA WAKE ZAO

Bingwa - - MAHABA -

KITENDO cha watu kuwa katika mahusiano ya kimapenzi kinatakiwa kitoe maana ya upendo katika ujumla wake unaostahili.

Watu wanaopendana kwa kawaida husikilizana, husaidiana, hutakiana heri na huoneana huruma. Yote hayo yanatakiwa kuonekana katika kauli za wahusika, ila hasa katika matendo yao.

Maana ya upendo wako kwa mwenzako daima haiwezi kuonekana kama unamfanya ajute na asiye na furaha na uwepo wako katika maisha yake ama na uamuzi wake wa kuwa na wewe.

Tafiti zinaonesha mbali na makosa kadhaa wanawake ambayo huwa wanayafanya kwa waume zao, ila wanaume wengi huwakosea mno wake ama wapenzi wao wanapoishi pamoja kiasi kwamba juu ya maisha yao huwezi kuona maana halisi ya upendo.

Mfano, wanaume wengi baada ya kuingia katika ndoa wanapenda kuishi na wake zao katika mtindo usio na tofauti sana na utumwa.

Yaani kwa kuwa mke yuko ndani, basi kila kazi inayohusu nyumba, usafi ama watoto, inamhusu yeye bila kujali kwa wakati huo yeye mwanamume anafanya kazi gani.

Ndugu zangu, maana ya upendo inatakiwa ionekane pia kwa namna unavyohisi uchovu wa mwenzako.

Ni kweli, kuna mgawanyo wa madaraka. Ni kweli kazi nyingi za nyumbani ni jukumu la kina mama. Ila je, umewahi kujiuliza toka aamke huwa anafanya kazi ngani na huwa anajisikiaje?

Ikiwa kweli unampenda na kumjali, utajiona una ulazima kama sio wa kumtafutia msaidizi wa ndani, basi hata wewe kujumuika naye katika kufanya kazi.

Upendo wake kwa mpenzi wako hauishii kuonekana chumbani tu ama katika kauli zako tu. Thamani na heshima ya upendo wako itaonekana katika kiwango cha huruma na kujali unachomuonesha.

Wanaume wengi wakiwa na wanawake wasioajiriwa ama kumiliki biashara, hudhani wanawake hao hukaa tu nyumbani hivyo kustahili kazi zote za hapo.

Hebu jiulize kwa makini, toka anaamka huwa anafanya kazi ngapi?

Wakati wewe unaamka asubuhi kwa ajili ya kwenda huko kazini, yeye huamka mapema kwa ajili ya kuweka sawa mazingira ya nyumba, kuwaandaa watoto, kuosha vyombo pengine na kusaficha zile nguo ulizovaa jana.

Wakati huo wewe upo ama katika gari lako, bodaboda ama daladala ukienda kazini. Ukifika huko, baada ya masaa takribani nane unakuwa njiani kurudi nyumbani.

Yeye anakuwa busy kuandaa chakula kwa ajili ya familia, kusafisha nyumba na ratiba nyingine za nyumbani.

Unafika nyumbani ukidai umechoka mno kwa majukumu ya kutwa nzima, haraka haraka, anakutengea maji kwa ajili ya kuoga, huku akiwa tayari kaweka chakula mezani ule baada ya kuoga.

Unamaliza kula, anatoa vyombo, anatandika kitanda, anakuandalia nguo kwa ajili ya kesho kazini.

Kumbuka toka asubuhi hakuwa na muda wa kupumzika kama ulio nao wewe baada ya kutoka kazini.

Ila kwa kuwa hana kazi ya kuajiriwa ama kumiliki biashara, yupo juha mmoja anayejiita mumewe anamuita goli kipa.

Uimara wa mahusiano yako unajengwa kutokana na namna unavyoonesha kumjali na kumheshimu mwenzako.

Mke wako ni sehemu muhimu ya maisha yako. Mke wako ni rafiki na sababu kubwa ya wewe, furaha na amani. Mheshimu, mjali na mtunze. Mke wako sio msaidizi wako wa kazi za ndani.

Wapo wanawake hata ikitokea wakatengana na waume zao kesho kwa sababu yoyote ile, bado wataendelea kuwakumbuka, na kutamani kuwa nao ama kuwa na wanaume wa sampuli hiyo.

Hayo mambo hayaji kwa bahati mbaya. Yanatokea kwa sababu wahusika waliacha alama muhimu katika maisha ya wandani wao.

Je, kuna alama gani unaiacha kwa mke wako? Vitu gani mke wako atamisi kama ikatokea ukasafiri ama kutengana?

Au atakuwa hana cha kukumbuka zaidi ya kushukuru kuondokwa na kero zako na maisha ya utumwa uliyomfanya akayaishi?

Inaongeza mvuto na bashasha katika mahusiano mume akimsaidia mkewe kazi za nyumbani. Mke hujiona hatumikishwi ila anapendwa.

Mke hujiona anathaminika na kuona alipo ni mahali sahihi zaidi.

Wanawake wengi walio katika ndoa hawana furaha kama ilivyokuwa enzi za uchumba ama urafiki wao na wahusika.

Kipindi cha uchumba walioneshwa kupendwa, kusikilizwa na kuthaminika. Ila baada ya kuingia katika ndoa kisha labda wakafanikiwa kuzaa, kwa wengi maisha huwa kama yanawageuka.

Wanatoka kuwa katika thamani waliyodhani wanayo na kuwa vifaa vya vyumbani vyenye kuletewa tu chakula, dawa vikiugua na matumizi mengine.

Hawasikilizwi wala kudekezwa kama ilivyokuwa zamani.

Kosa hili walifanyalo wanaume wengi baadaye hugeuka fimbo ya kuwachapia kama wanawake husika wakikutana na waume wengine watakaowafanya wahisi wa thamani na maana katika maisha yao.

Wanawake wengi wenye kuishi katika mahusiano ilimradi ama ndoa ndoano, hujikuta wakikubali kuwa na wanaume hao na kuwapotezea kabisa wanaume zao wa awali.

Acha kuishi kimazoea, mfanye mke wako ajione kabahatika kuwa na wewe na si kujiona alikuwa mjinga kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na wewe.

Kumbuka toka asubuhi hakuwa na muda wa kupumzika kama ulio nao wewe baada ya kutoka kazini. Au atakuwa hana cha kukumbuka zaidi ya kushukuru kuondokwa na kero zako na maisha ya utumwa uliyomfanya akayaishi?

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.