MBELGIJI AWACHEMSHIA DAWA JJUUKO, WAWA

Bingwa - - HABARI - NA ZAITUNI KIBWANA

HUENDA mabeki wa Simba, Jjuuko Murshid na Pascal Wawa wakawa kwenye mazingira magumu ya kupata namba kutokana na mpango wa Kocha Mkuu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Patrick Aussems wa kusaka beki mwenye ubora zaidi yao.

Wakati dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu, Aussems ametaja nafasi tatu ambazo anahitaji kuziongezea nguvu ndani ya kikosi hicho ikiwamo safu hiyo ya ulinzi.

Kocha huyo yupo katika mkakati kabambe wa kuboresha kikosi chake kwa ajili ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kuanza Desemba mwaka huu.

Akizungumzia mikakati yake hiyo jana asubuhi baada ya kumalizika kwa mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veterani, jijini Dar es Salaam, Aussems alisema amekiangalia kikosi chake kwa upana na kugundua anahitaji kupata kiungo, mkabaji, mshambuliaji na beki mmoja wa kati ili kukidhi mahitaji yake.

Katika mipango hiyo, Aussems alisema hatagusa eneo la kipa kwani makipa wa sasa Aishi Manula, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Said Mohammed ‘Nduda’, wanamtosha.

“Bado naangalia wachezaji sijajua nitawapata wapi ila natafuta kuanzia kiungo, mshambuliaji na beki isipokuwa nafasi ya kipa ndio ambayo sitagusa,” alisema Aussems.

Aussems alipotakiwa kutaja orodha ya wachezaji atakaowaacha na wengine kutolewa kwa mkopo kuwa ni Marcel Kaheza, Rashid Juma, Ali Abuu, Abdul Hamis, Nicolas Gyan, Vicent Costa na Salim Mbonde ambaye amekuwa majeruhi wa muda mrefu.

Pia kocha huyo ameonyesha kukerwa na tabia ya ubinafsi kwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ambao wanaojiona ‘mafaza’ na kushindwa kuwa na umoja.

Katika mazoezi hayo, kocha huyo alisikika akiwaambia wachezaji hao kuwa wanapambana kwa ajili ya timu na si faida ya mtu binafsi.

“Tunafanya mazoezi kwa ajili ya manufaa ya timu, lazima tufanye kazi kwa pamoja na si kila mtu anafanya anachotaka hatuwezi kufika,” Aussems alisikika akiwaambia wachezaji hao.

Katika mazoezi hayo ya jana yaliyoanza saa 3:00 asubuhi hadi 11:00 asubuhi, kocha huyo alionekana kuwapa wachezaji wake mbinu za kufunga, ambapo programu hiyo iliwahusisha wachezaji wote wakiwamo mabeki, viungo na washambuliaji ambao hawajaitwa kwenye timu za taifa kama Marcel Kaheza, Mohammed Rashid na Rashid Juma.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.