Magufuli ampasua kichwa Amunike

Bingwa - - HABARI - NA MWAMVITA MTANDA

KAULI ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli,

imeendelea kumpasua kichwa Kocha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Emmanuel Amunike.

Mwezi uliopita, Dk. Magufuli aliita timu hiyo Ikulu na kumwagiza Amunike afanye maandalizi mazuri ili aweze kushinda au kutoka sare katika mechi yao ya kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon 2019) dhidi ya Lesotho, akisema anamwamini na ana imani Stars itashinda.

Kutokana na kauli hiyo, Amunike amekuwa akiiwaza mechi hiyo ili kuhakikisha hamwangushi Magufuli, kwa kuwa amesema anamwamini.

Akizungumza na BINGWA juzi, Amunike alisema ana kibarua kizito cha kuhakikisha kuwa timu yake inarudi na ushindi.

“Natambua kuwa naweza kuisaidia timu kufanya vizuri, lakini pia siko tayari kumwangusha Mheshimiwa kwa juhudi alizozifanya za kuisapoti timu na Watanzania kwa ajumla ambao kwa sasa akili zao zinawaza michuano hiyo ya Afcon,” alisema Amunike.

Amunike alisema katika kipindi hiki ambacho timu yake inaingia kambini, atakuwa na wakati mzuri wa kurekebisha mapungufu machache na kuiandaa timu hiyo kwa mechi hiyo itakayochezwa Novemba 18, mwaka huu nchini Lesotho.

Kocha huyo alisema Watanzania wasiwe na hofu yoyote juu ya mchezo huo, kuna asilimia kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na ubora wa kikosi chake.

“Matumaini ya kurudi na ushindi yapo kwa asilimia nyingi, nasema hivyo kutokana na ubora wa kikosi changu, mimi ni mwalimu, kazi yangu ni kuwapa maelekezo, pia nao wana nia moja ya kushinda,” alisema Amunike, ambaye kwa sasa yuko na kikosi hicho nchini Afrika Kusini kwa ajili ya maandalizi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.