Urafiki Shooting wapeta Ligi ya Ubungo

Bingwa - - HABARI - NA VALERY KIYUNGU

TIMU ya soka ya Urafiki Shooting ya Ubungo, juzi iliwafunga vibonde Street Worriers ya Goba mabao 3-0, katika mechi ya hatua ya pili ya Ligi Daraja la Tatu Wilaya ya Ubungo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam.

Street Worriers ambayo imepata matokeo ya kusuasua katika ligi hiyo, ilijaribu kujitutumua kipindi cha kwanza hadi kwenda mapumziko ikiwa haijaruhusu bao lolote.

Katika mechi za hatua ya awali, timu hiyo iliwahi kufungwa mabao 7-1 dhidi ya Ubungo Terminal FC.

Katika mechi hiyo ya juzi, washindi walifunga mabao yote kipindi cha pili na wafungaji ni Daniel Mwainjekula, Ramadhani Mangosi na Ally Mkoko.

Hata hivyo, timu zote zilianza mchezo kwa kasi ya kushambuliana kwa zamu, ambapo dakika ya 15 Street Worriers walikosa bao la wazi.

Mechi nyingine zitapigwa leo ambapo Dago Stars ya Mburahati itavaana na Songas ya Ubungo kwenye Uwanja wa Huduma Kibangu, Sisi kwa Sisi watamenyana na Kiluvya Uwanja wa Kinesi, huku Makongo wakichuana na Kibanda katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ukombozi.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.