Pawasa aahidi kuwavua ubingwa Senegal

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - NA MWAMVITA MTANDA

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya soka la ufukweni, Boniface Pawasa, amesema kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka na ushindi na kuwavua ubingwa Senegal, katika michuano ya Mataifa ya Afrika inayotarajia kuanza Desemba 8 hadi 14 nchini Misri.

Timu hiyo tayari ilishaanza mazoezi yake tangu Novemba 3 katika Fukwe za Coco ikiwa na jumla ya wachezaji 18, imepangwa kundi B lenye timu hiyo ya Senegal, Nigeria na Libya.

Akizungumza na BINGWA jana, Pawasa alisema ni wakati wa kufanya mabadiliko na kuhakikisha timu yake inaibuka na ushindi, ili kuendelea kuitangaza nchi kwa matokeo mazuri.

“Kuna wakati lazima tujihakikishie kila jambo linawezekana, tunaweza kuwavua ubingwa Senegal kwa juhudi zetu na kutokana na ubora wa kikosi cha mwaka huu naamini kabisa tutashinda na kurudi nyumbani kwa furaha kubwa,” alisema Pawasa.

Pawasa alisema timu yake haijawahi kuleta matokeo ya kuridhisha katika michuano hiyo, kutokana na kuwa wageni na timu wanazokutana nazo, tofauti na msimu huu tayari baadhi ya timu walishakutana nazo na watambua mbinu zao hivyo ni rahisi kupambana nao.

Pawasa alisema timu yake kwa sasa ipo kambi ya wazi, lakini hivi karibuni ataweka bayana juu ya kambi rasmi ya kikosi hicho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.