Pacha wa Makambo apatikana Yanga

Bingwa - - HABARI /TANGAZO - NA ZAINAB IDDY

STRAIKA wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, amesema ili timu hiyo ifunge mabao mengi mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania ni lazima kocha Mwinyi Zahera, ampe nafasi mshambuliaji wa Mbeya City, Eliud Ambokile, atakayetengeneza pacha na Heritier Makambo.

Katika msimu huu wa ligi, Yanga imeonekana kupata ushindi kiduchu katika michezo yake, kwani katika michezo 10 iliyocheza wamefunga mabao 17 huku watani zao Simba wakiwa na 23 mechi 11.

Akizungumza na BINGWA jana, Mmachinga, alisema hadi sasa Yanga ina mapungufu sehemu ya ushambuliaji na mtu pekee atakayeleta faraja ni Ambokile.

“Makambo anahitaji pacha wa kusaidiana naye kwenye upachikaji mabao nje na Ibrahim Ajib, hivyo litakuwa jambo bora safu ya ushambuliaji akiongezwa Ambokile katika usajili wa dirisha dogo.

“Msimu uliopita niliwahi kusema Ambokile anahitajika Yanga, lakini nikapuuzwa na leo narudia Zahera atafanya makosa iwapo akisajili straika wa Tanzania, ambaye si mchezaji huyo mwenye kipaji cha aina yake kwenye ufungaji,” alisema na kuongeza:

“Mbali na uhitaji wa straika walionao Yanga, lakini pia dirisha dogo ni jambo zuri kuongeza wachezaji katika nafasi ya winga na beki watakaoleta mafanikio na hata kusaidia kutwaa taji la ligi.”

Katika mbio za ufungaji bora, Ambokile anaongoza akiwa na mabao nane akifuatiwa na Emmanuel Okwi na Meddie Kagere, wanaokipiga Simba.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.