KIPAUMBELE YANGA NI UCHAGUZI, WASIOTAKA WAKAE PEMBENI

Bingwa - - MAONI | MTAZAMO | KATUNI -

HIVI karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Yanga kutokana na baadhi ya viongozi wake kujiuzulu nafasi zao.

Uchaguzi wa Yanga umepangwa kufanyika Januari 13 mwakani, ambapo wanachama watapiga kura kuchagua viongozi watakaojaza nafasi zilizoachwa wazi.

Hata hivyo, mchakato wa uchaguzi wa Yanga haukufanyika mapema kutokana na baadhi ya wanachama kutaka aliyekuwa Mwenyekiti wao, Yussuf Manji arejee, lakini hakuonyesha ushirikiano.

Kulikuwepo na mvutano wa muda mrefu tangu klabu hiyo kutakiwa kuitisha uchaguzi wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi mpaka viongozi wa klabu hiyo walipokutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, kujadili suala hilo kwa kina.

Lakini pia baadaye Baraza la Michezo la Taifa (BMT), lilikuja na uamuzi wa kuitaka TFF isimamie klabu hiyo ifanye uchaguzi.

Nafasi zinazotakiwa kujazwa katika uchaguzi huo ni pamoja na mwenyekiti, makamu mwenyekiti na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji.

Kutokana na hali halisi iliyopo ndani ya klabu hiyo kwa sasa, hakuna sababu ya baadhi ya wanachama kuibuka na kuzungumzia mambo yasiyokuwa na manufaa kwa uchaguzi kwani yanaweza kuukwamisha.

BINGWA tunaamini timu ya Yanga inaweza kufanya vizuri hata katika Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa uchaguzi utafanyika na kupatikana viongozi bora ambao wana weledi wa kufanya kazi kwa ufanisi.

Ikiwa klabu hiyo itapata watu sahihi wa kuongoza, mambo huenda yakabadilika na kuanza kuwa na mwelekeo mzuri katika suala zima la kujiendesha kiuchumi na kupata mafanikio.

Tunaamini viongozi ndio kila kitu katika kuhakikisha malengo ya klabu yanafanikiwa, hivyo huu ni wakati wa wanachana kukaa chini na kutuliza akili zao, wakitafakari kile ambacho wanakihitaji ndani ya klabu yao.

Viongozi wote wanaojitosa kutoa michango yao ili kufanikisha jambo hili hakika wana nia njema ya kuisaidia klabu ya Yanga kutoka ilipo na kupiga hatua kubwa mbele, hivyo hata wanachama wanapaswa kuonyesha ushirikiano wao wa dhati.

Jumapili iliyopita watani wao wa jadi, Simba walifanya uchaguzi na kupata viongozi wapya ambao wataongoza kwa miaka minne ijayo.

BINGWA tunapenda kutoa rai yetu kwa wanachama wa Yanga kwamba suala la uchaguzi ni muhimu na halikwepeki, hivyo ni vyema wakatulia na kuiga mfano wa mahasimu wao ambao tayari wamewaacha mbali baada ya kuingia kwenye mfumo mpya wa uendeshaji.

Kwa sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri kwa upande wa Simba kutokana na mfumo mpya walioingia, hivyo ni muhimu Yanga nao wakafuata njia sahihi ambazo zitawawezesha kupiga hatua.

Hakuna ubishi kwamba ili klabu yoyote ifanikiwe ni lazima iwe na viongozi sahihi wanaojitambua na kuelewa majukumu yao, hivyo suala hili la uchaguzi linalosisitizwa lina umuhimu mkubwa.

Tunaona ni vyema wale wasioitakia mema klabu ya Yanga wakae pambeni kupisha mchakato huo ufanyike kwa umakini bila kuwepo kwa migogoro isiyokuwa na tija.

Kutokana na umuhimu wa jambo hili, BINGWA hatuna budi kulisisitiza kwa wanachama wa Yanga ili nao watambue kwamba ushirikiano wao unahitajika katika kufanikisha uchaguzi huo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.