RONALDO AWATULIZA JUVENTUS

Bingwa - - MBELE - ROMA, Italia

NYOTA wa Juventus, Cristiano Ronaldo, amewataka mastaa wenzake kutulia kufuatia kipigo walichokipata juzi dhidi ya Manchester United katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Katika mtanange huo uliopigwa mjini Turin, Ronaldo aliweza kupachika bao lake la kwanza katika mashindano hayo akiwa na vinara hao wa Serie A, lakini halikuweza kuwanusuru na kipigo hicho licha ya kutawala mchezo dakika zote.

Mpira wa adhabu uliopigwa na Juan Mata, ndio ulifanya ishuhudiwe Man Utd wakipata bao la kusawazisha kabla ya beki wa Juventus, Alex Sandro, kujifunga na kuwafanya mashetani hao wekundu kuondoka uwanjani kifua mbele na ushindi huo wa mabao 2-1 katika mcezo huo wa Kundi H.

Hata hivyo, pamoja na kipigo hicho cha kwanza baada ya kushinda mechi 15 msimu huu, Ronaldo anasisitiza kwamba hakuna sababu kwa Juve kushikwa na kiwewe.

"Lilikuwa ni bao zuri sana baada ya kupokea vizuri pasi kutoka kwa Leonardo Bonucci, lakini halikutosha," straika huyo aliuambia mtandao wa UEFA.com.

"Najipongeza kwa kuweza kufunga bao langu la kwanza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya nikiwa na Juventus na tulikuwa vizuri. Ila tumeendelea kuongoza kwenye kundi letu hivyo hakuna haja ya kuanza kuingiwa kiwewe,” aliongeza staa huyo. Pamoja na kufungwa, Juve wanaendelea kukaa kileleni mwa kundi hilo wakiwa na pointi tisa wakifuatiwa na Man Utd yenye pointi saba, Valencia ni ya tatu ikiwa na pointi tano na ya mwisho ni Young Boys yenye moja.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.