Yanga yajizatiti Kanda ya Ziwa

Bingwa - - HABARI - NA HUSSEIN OMAR

HII huenda ikawa isiwe habari njema kwa Mwadui FC na Kagera Sugar, kutokana na benchi la ufundi la Yanga kuamua kwa kauli moja kuweka mikakati kabambe itakayowawezesha kuwasambaratisha na kuzoa pointi zote sita kutoka Kanda ya Ziwa.

Yanga wanafahamu kuwa ushindi huo wa ugenini ndio utakaowazesha kurejea kwenye kasi yao ya kutaka kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini pia kuwatambia wapinzani wao hao ambao wamekuwa wakisumbua kila wanapokutana.

Kwa kufahamu hilo, mbali na mikakati ya klabu kwa ujumla, benchi la ufundi la Yanga likiongozwa na Mwinyi Zahera limeomba mechi mbili za kirafiki, moja ya kimataifa, kwa ajili ya kuwaweka sawa wachezaji wake, lengo likiwa kuibuka na ushindi katika michezo yake hiyo miwili ya ugenini.

Iwapo Yanga watashinda michezo hiyo miwili, watafikisha pointi 32, hivyo kuwakaba koo Azam, walio kileleni na Simba wakiwa nafasi ya pili kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Ratiba inaonyesha kuwa Yanga itakuwa wageni wa Mwadui FC Novemba 22, katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, kabla ya kuifuata Kagera Sugar katika mchezo utakaochezwa, Novemba 25, Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Akizungumzia juu ya mikakati hiyo mratibu wa kikosi hicho, Hafidh Saleh, aliliambia BINGWA kuwa, michezo hiyo ni muhimu kwa kikosi chao, kwani itasaidia kuwaweka sawa vijana wao kwa ajili ya kuwania pointi sita katika mechi mbili za ugenini.

Alisema wako katika hatua za mwisho za kuileta moja ya timu zinazofanya vizuri kwenye ligi ya Malawi, ili iwape changamoto vijana wao kabla ya kucheza nje ya Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu msimu huu ulipoanza.

“Ni kweli tupo katika hatua nzuri ya mazungumzo na kuileta timu hiyo ya Malawi, hatuwezi kuiweka wazi kwa sasa kwa kuwa taratibu bado hazijakamlika.

“Kama tutafanikiwa kucheza michezo hiyo, itatusaidia kuwajenga wachezaji wetu kisakolojia kwa ajili ya kusaka pointi sita ugenini, tunakwenda Kanda ya Ziwa ambako ni kugumu kupata pointi tatu, lakini kwa mikakati hii tuliyoiweka tunaamini tutaondoka na pointi zote sita,” alisema Saleh.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.