Okwi, Pluijm watu bora Oktoba

Bingwa - - HABARI - NA MWAMVITA MTANDA

SHIRIKISHO la Soka Tanzania ‘TFF’, limemtangaza mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, kuwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba mwaka huu.

Okwi, ambaye tayari ameshafikisha idadi ya mabao 7 na kufunga hat-trick msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu uliopita alibeba kiatu cha dhahabu akiwa na idadi ya mabao 20.

Akizungumza na BINGWA, Msemaji wa Shirikisho hilo, Clifford Ndimbo, alisema kuna kiasi cha pesa ambacho kimeandaliwa kwa ajili ya zawadi ya mchezaji huyo, kwa lengo la kuhamasisha wachezaji waendelee kufanya vizuri.

Ndimbo alisema, mchezaji bora wa mwezi Agosti, Meddie Kagere naye aliandaliwa zawadi ya Sh milioni moja, hivyo Okwi naye atazawadiwa.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van De Plujim, naye ameibuka kuwa kocha bora mwezi Oktoba, akiwapiku makocha wa klabu zote 20 zinazoshiriki ligi.

Pluijm anaiongoza vema klabu yake ya Azam, ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi 30.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.