Sakata la Humud lachukua sura mpya

Bingwa - - HABARI - NA ZAITUNI KIBWANA

SIKU chache baada ya klabu ya KMC kutangaza kuachana na kiungo wake, Abdulhalim Humud, mwenyewe ameibuka na kusema meneja wake, Antonio Nugaz, anaangalia namna ya kufanya ili haki itendeke.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, amefukuzwa KMC kwa madai ya kutaka kutembea na wake pamoja na wapenzi wa wachezaji wenzake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Humud, alisema viongozi wa KMC wameamua kumchafua tu wanapaswa kusema ukweli.

Humud aliyewahi pia kuzitumikia Coastal Union na Azam FC, alisema aliandika barua mwenyewe ya kuomba kuachwa na KMC, baada ya kuona anakosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Etienne Ndayiragije.

“Mimi ni mchezaji ili nionekane kuwa bora lazima nicheze, siridhiki kuchukua mshahara bure bila kuutumikia popote ndio maana niliandika barua mwenyewe ya kuomba niachwe.

“KMC walikubali ila kwa masharti ya kurudisha jezi na vifaa vyote walivyonipa, wakasema watamtafuta mwanasheria wao ili waangalie kama kuna sehemu natakiwa kulipa kwa sababu mimi ndio nimeomba kuvunjiwa mkataba,” alisema.

Alisema anashangaa baada ya barua hiyo, wanaibuka na kusema nimechukua wake za wachezaji wenzangu, huku ni kunichafua kwa kuwa hizi ni tuhuma nzito.

“Najiuliza hizi ndizo fadhila zangu za kuipandisha timu? Sipati jibu kwa sababu bao langu la kichwa nililofunga ndio liliipelekea KMC kufika hapa, wameamua kunichafua ila nawaambia mimi sitakosa timu ya kucheza kwa uwezo wa Mungu.

“Alafu hao wake za wachezaji wenzangu mimi wa kazi gani, niseme tu nina mke mzuri na sihitaji wengine hizo ni njama za kunichafua tu,” alisema.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.