KAHEZA, MO RASHID KUTUA COASTAL UNION

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI - NA OSCAR ASSENGA, TANGA

MASTRAIKA wawili kutoka klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Marcel Kaheza na Mohamed Rashid ‘Mo’, huenda wakatua kwa mkopo katika kikosi cha timu ya Coastal Union maarufu Wagosi wa Kaya, wakati wa dirisha dogo la usajili.

Hatua hiyo inatokana na uongozi wa klabu ya Coastal Union kuiandikia barua Simba kuwaomba wachezaji hao ili kukiongezea nguvu kikosi chao.

Mwenyekiti wa klabu ya Coastal Union, Steven Mnguto, alilithibitishia BINGWA jana kuwa ni kweli wameandika barua hiyo na wanasubiri majibu ili kujua kama watafanikiwa kuwapata.

Aidha, alisema anaamini suala hilo litakwenda vyema ili wachezaji hao waruhusiwe kukitumikia kikosi hicho cha Wagosi wa Kaya katika mechi zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Kwa sasa tuna mpango wa kuwasajili kwa mkopo Kaheza na Mohamed Rashid katika dirisha dogo la usajili, tayari tumeanza kufanya taratibu kwa kuiandikia barua Simba kuwaomba wachezaji hao,” alisema.

Hata hivyo, aliongeza kwamba baada ya kupokea ripoti ya kocha mkuu, Juma Mgunda, wataanza kuyafanyia kazi kwa kusaka wachezaji watakaopendekezwa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.