FANYA HIVI ILI AWEZE KUELEWA HISIA ZAKO VEMA

Bingwa - - MAHABA - NA RAMADHANI MASENGA ramadhanimasenga@yahoo.com, Instgram: ramadhan.masenga 0719 053327

INATOKEA unakuta kijana analalamika kwamba kila akimwambia fulani hisia zake haelewi. Yaani anamwambia kila neno, hata anamlilia na kumpigia magoti, ila bado hisia zake hazithaminiwi. Na wewe upo katika kundi hilo?

Na wewe kuna mtu hakuelewi kila unapomwambia unamuhitaji na kutaka kumfanya awe mpenzi wako? Acha kupoteza muda wako. Fikiria suala hili.

Tambua mtu haingii katika mahusiano ya kimapenzi kwa sababu ya wewe kulia sana ama kwa sababu unatia sana huruma. Hapana. Mtu anaingia katika mahusiano ya kimapenzi baada ya kuhisi wewe ni mtu mwafaka kwake ambaye utampa faraha, amani na raha. Je, umemsoma mwenzako kabla ya kwenda kumlilia na kuhitaji kuwa mpenzi kwake?

Kutongoza ni suala la mchakato (process), si suala la kumwambia tu mtu hisia zako na yeye akukubali haraka. Hapana. Hiyo si njia nzuri sana. Njia sahihi kwanza ni kumsoma mtu na kujua nini anataka na nini hapendi. Ukimsoma kwa muda mrefu na kujua udhaifu wake hapo ndio unaweza kwenda kutega mitego yako.

Kabla hujafunua kinywa chako na kumweleza namna unavyompenda na kumhitaji katika maisha yako, inabidi kupitia matendo na maisha yako avione vitu anavyotaka katika maisha yake.

Binadamu ni viumbe wabinafsi sana. Mtu hawi na mtu kwa ajili ya shida ya mtu mwingine. Mtu anaingia katika mahusiano baada ya kuona kuna kitu atapata na nafsi yake itatulia. Acha kupoteza maneno yako bure. Jiulize, kwanza unamjua vizuri mwenzako? Unafahamu udhaifu na uimara wake?

Ikiwa unautambua udhaifu wake, inabidi utumie nafasi hiyo kumvuta kwako. Kama unajua mhusika (target) anapenda sana mwanamume mwenye kubembeleza na kudekeza, kwa kutumia akili na ubunifu, inabidi umfanye ajue wewe ni mwanamume wa aina hiyo. Kama umegundua mwenzako anapenda sana wanaume watanashati na wenye uelewa mkubwa, kwa umakini mkubwa inabidi akuhisi wewe ni mtu wa namna hiyo.

Kutongoza si maneno tu. Mtu hawi na mtu kwa sababu anayemtongoza ana shida naye sana. Mtu anakuwa na mtu baada ya kuhisi furaha yake, amani yake na burudani yake itakuwa ya uhakika kama akiwa na fulani. Kutokana na ubinafsi wa binadamu, watu hawawi na shida ya matatizo na mwingine, ila wanawaza zaidi shida na matatizo yao. Acha kutupa maneno yako bure, acha kwanza kulialia ukiamini kwa kufanya hivyo mwenzako atakuelewa na kukubali, wewe fanya aone matatizo yake yatakuwa na ukomo ikiwa atakuwa na wewe. Kwa tamaa ya furaha, amani na raha, ataanza kukuona wewe ni mtu mwafaka. Atakufikiria, atakuwaza na kutamani siku ifike uinue mdomo wako na kusema unampenda ili akukubalie kwa nderemo na vifijo. Ila kumbuka pupa ni adui yako namba moja katika kutekeleza suala hili.

Kila tukio unalofanya inabidi ulifanye kwa akili na hesabu kubwa. Mfano, ili ujue yeye ni mtu wa aina gani inabidi uanzishe naye urafiki. Urafiki huu inabidi uwe wa muda mrefu na mara nyingi usizungumzie masuala ya mapenzi kabisa.

Mwanamke akikutana na mwanamume kwa mara ya kwanza hudhani mwanamume husika ana lengo la kumtongoza na hivyo kujiandaa kupambana naye ili asionekane wa bei rahisi. Kuepuka kadhia hii, wewe acha kabisa kuzungumzia masuala ya kimapenzi na kuwa kawaida sana kwake.

Muda mwingi wa urafiki wenu, penda kuwa mchokozi wa mada, kisha mwache yeye awe mzungumzaji mkuu. Katika kuzungumza sana kwake ndipo utajua uwezo wake wa kufikiri, vitu anavyopenda na vitu anavyochukia.

Utavijua vitu anavyochukia kwa kupenda kuvizungumzia katika namna hasi (negative) na utajua vitu anavyopenda kwa kupenda kuvisifia ama kuvizungumzia mara kwa mara. Pia hakikisha baada ya kuanza kumsoma na kumwelewa, na wewe uwe unazungumzia vitu anavyopenda. Hii itamfanya apende kuwa karibu na wewe pamoja na kukusikiliza. Hakuna mtu ambaye hapendi kuwa karibu na mtu mwenye kuzungumzia vitu anavyopenda. Hata marafiki wamekuwa marafiki kwa sababu muda mwingi hupenda kuzungumzia vitu ambavyo vinawafurahisha wakivisikiliza. Mwenzako atajisahau na kujikuta anaanza kukuhitaji ikiwa utakuwa huna pupa na uko makini katika kuratibu mambo yako. Pia acha kuamini kuwa kukaa naye muda mwingi mkizungumza ndipo kutafanya akupende sana. Hapana. Kukaa naye muda mwingi na kupiga stori kutamfanya akuzoee mapema kisha akukinahi. Jifunze kujua muda gani wa kumkwepa na muda gani wa kuwa naye. Si kila muda unapokutana naye uongee naye sana mpaka stori ziishe, hapana. Epuka kitu hicho. Kuna wakati hata akiwa na hamu ya kukaa na wewe, epuka kukaa naye. Inabidi umpe muda wa kukumisi na kukutafakari. Namna avyokufikiri ndivyo namna atakavyokuwa anakuhitaji zaidi. Kitendo hicho kitarahisisha hata jitihada zako za kutaka kumuingiza katika himaya yako. Kuna watu huamini kuwa kukaa muda mwingi na wanaowataka watawafanya kupendwa, ni uongo. Huko hakukufanyi upendwe, ila kutafanya aanze kujua madhaifu yako mapema na kupoteza msisimko na wewe. Kuwa makini katika hatua zako za kutimiza lengo. Pupa ama kujisahau kwa namna yoyote kunaweza kukupotezea windo lako. Instagram:ramadhan. masenga ramadhanimasenga@yahoo.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.