Kocha Alliance afunguka siri ya ushindi

Bingwa - - MAONI MTAZAMO KATUNI - NA DAMIAN MASYENENE, MWANZA

KOCHA wa muda wa kikosi cha Alliance FC, Gilbert Daddy, amefunguka na kuweka wazi kinachoiwezesha timu yake kupata matokeo ya ushindi katika Ligi Kuu Tanzania Bara tofauti na nyuma.

Katika michezo mitatu aliyoiongoza timu ya Alliance, ameiwezesha kushinda miwili na kupata sare moja hivyo kujinasua mkiani mwa ligi.

Daddy aliikuta timu hiyo inaburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi sita, lakini ameisaidia kuvuna pointi saba katika michezo mitatu na kupanda hadi nafasi ya 16.

Akizungumza baada ya kushinda dhidi ya Mtibwa Sugar juzi kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza, Daddy alisema kikosi hicho kimeanza kupata matokeo baada ya kujua namna ya kuwatumia wachezaji waliopo.

Alisema pia amekuwa akiwahamasisha kujua hadhi na wajibu kila wanapokuwa uwanjani.

Tangu kocha huyo atue kikosini hapo, baadhi ya wachezaji wamebadilishiwa majukumu yao uwanjani akiwamo Siraji Juma ambaye awali alikuwa straika na sasa anacheza kama beki wa kushoto.

Pia kiungo mshambuliaji, Juma Nyangi, amerudishwa kuisaidia safu ya ulinzi na kukifanya kikosi hicho kubadilika kila mara.

"Ushindi huu ni muhimu kwetu na unawafanya wachezaji wajiamini, wamecheza vizuri hivyo tulistahili pointi tatu, kama kocha ninajua nani anafaa sehemu gani na wapi nimtumie.

"Hakuna maajabu yanayofanyika ili timu ipate ushindi, kikubwa ni kuhamasisha vijana wajue hadhi na wajibu wao uwanjani," alieleza.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.