Mayweather akana kuzipiga na Nasukawa

Bingwa - - HABARI - NEW YORK, Marekani

BONDIA Floyd Mayweather, amesema kwamba hajaingia makubaliano yoyote ya kupigana pambano la ngumi na mateke ‘kickboxer’ dhidi ya Mjapan, Tenshin Nasukawa, ambalo linadaiwa litafanyika wakati wa sikukuu ya mwaka mpya.

Bingwa huyo wa dunia ambaye hajawahi kupigwa, anadaiwa kuingia makubaliano na makampuni ya RIZIN Fighting Federation, lakini anachodai ni kwamba, makubaliano waliyofikia ni kupanda ulingoni kwa muda wa dakika tisa za raundi tatu na bondia ambaye hakumtaja.

Kwa mujibu wa taarifa hizo za awali, Mayweather, anadaiwa kuwa angetangaza pambano hilo dhidi ya Nasukawa Jumatatu ijayo akiwa mjini Tokyo nchini Japan, lakini anazikana taarifa hizo akidai kwamba hajawahi hata kusikia kuwapo kwa pambano hilo.

Staa huyo raia wa Marekani, alisema kuwa ameshtushwa kuwapo maandalizi ya pambano hilo bila hata yeye kuwa na taarifa.

"Kwa sasa nimesharejea kwenye ardhi ya Marekani, baada ya safari ndefu na ya kuchosha mjini Tokyo, kwa sasa ni muda wa kuwaambia nyinyi mashabiki wangu kuhusu pambano linalodaiwa litakuwapo Desemba 31 mwaka huu,” aliandika kupitia ujumbe ambao aliutuma kwenye mtandao wake wa Instagram.

"Kwanza kabla ya yote niwaweke wazi mimi Floyd Mayweather, kamwe sijawahi kuingia makubaliano rasmi ya kupambana na Tenshin Nasukawa. Na ukweli pia ni kwamba sijawahi kumsikia hadi safari hii nilipokwenda Japan.”

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.