Tajiri wa masikini

Bingwa - - HADITHI - Ilipoishia

SASA ENDELEA Ni mimi Vanuell Banguwi,” nilijitambulisha. Macho yalimtoka alibaki ameduwaa asiamini kabisa kama ni mimi yule yule masikini wa Adorra, baadaye alinitazama vizuri kisha akasema.

Kila sehemu niliyokuwa nimepita nilikuwa nimeacha maswali mazito, hata walinzi wa mwanzo hadi wa karibu na lango, walistaajabu mwonekano wangu kiasi cha wengine kunisahau wasijue si mimi yule kijana Vanuell Banguwi niliyekuja mara mbili mahali hapo.

Mlinda lango aliponiona, aliniuliza mimi nani huku safari hii akiuliza kwa nidhamu kidogo maana mwonekano wangu mzuri ulimfanya asijue kuwa ni mimi yule yule aliyekuwa akinionyesha dharau kubwa.

Nilipojitambulisha alibaki ameduwaa, alipogundua kuwa ni mimi yule yule masikini aliendeleza dharau yake.

“Naona leo umepitiwa na neema bila shaka umepata kazi ndani ya himaya hii tukufu ndio maana hata mwonekano wako umebadilika,” aliongea.

Sikuongeza neno lolote juu ya hayo maneno yake, nilimwomba kuelekea kwa yule dada. Aliniruhusu nami nilianza kupiga hatua kuelekea eneo kuu la hekalu la tajiri Alexender. Baada ya dakika sita nilifika eneo tulivu na kusimama nje ya chumba cha yule dada ambaye ni bosi wangu kwa wakati huo.

Aliponiona aliniruhusu kuingia tofauti na siku zote ambazo huwa anasimamisha kama sanamu na kwa muda mrefu mlangoni, siku hiyo niliingia na kusimama mbele yake, upesi aliniruhusu kukaa. Alinitazama sana na kuniuliza.

“Karibu kwa Alexender Rugoa sijui nikusaidie nini?” aliniuliza kiasi cha kuniacha na mshangao mkubwa.

Ina maana kuwa alikuwa ameshindwa kunitambua kuwa mimi ndiye yule yule Vanuell Banguwi mtunza bustani.

“Waaaoo! Umebadilika nadhani mwonekano wako halisi ulijificha kutokana na umasikini wako.”

Nilitabasamu kwa kujilazimisha kisha nikasema.

“Nashukuru kwa msaada wako bosi wangu.”

Hakusema kitu tena alichukua karatasi na kuniambia nitie sahihi sehemu fulani iliyokuwa na onyesho la kuanza kazi. Baada ya kufanya hivyo aliniambia.

“Vifaa vyote viko hapo chini chumba cha pembeni unaweza kwenda kuanza kazi.”

“Nashukuru sana bosi wangu,” niliongea kwa nidhamu.

Nilisimama na kukiinamisha kichwa changu mara mbili mbele yake na kuondoka ofisini kwake, nilitoka pale na kwenda kwenye chumba cha pembeni kilichokuwa na kila kifaa cha bustanini, nilibeba mkasi mdogo na mkubwa, kijembe kidogo na vifaa vingine viwili.

Nilitembea kwa hatua kadhaa hadi kufika katika mlango wa kuingilia bustanini, sehemu iliyokuwa wazi yenye maua ya kila aina. Ilikuwa ni mara yangu ya pili kukanyaga bustani hiyo iliyokuwa mfano wa bustani ya Edeni. Lakini nilijiona kama nimefika kwa mara ya kwanza maana uzuri wake uliongezeka japo hakukuwa na mtunzaji kwa wakati huo.

Niliingia nikipiga hatua za taratibu, nilianza kufikiria sehemu ya kuanza kazi yangu, lakini kabla sijaanza nilijikuta namkumbuka yule msichana niliyemwona kwa mara ya kwanza humo msichana aliyekuwa mfano wa malaika. Kutokana na kuwa kwenye akili yangu mara zote, nilihitaji kumwona kwani toka siku ile sikuwa nimemtia machoni.

Nilitembea umbali mrefu kidogo nikielekea sehemu niliyokuwa nimemwona kwa mara ya kwanza. Sehemu yake iliyokuwa nzuri zaidi kuliko zote ndani ya bustani hiyo yenye ukubwa wa mita 100. Mahali alipokuwa akipumzika kulikuwa na kijani kibichi na maua ya kila rangi, vipepeo vya kila aina na ndege wanaotembea na kuruka.

Nilipofika ile sehemu, macho yangu yalinitoka zaidi maana nilimwona tena, mapigo yangu ya moyo yalianza kunisumbua yakikimbia sana, kama kawaida yake alikuwa akisoma kitabu. Nilijificha kwenye mmea ule ule mkubwa mfano wa mwavuli ili nipate kumfaidi. Ubongo, macho na moyo wangu vyote vilihamia kumtazama yeye, hakika nilizidi kustaajabu uzuri wake, uzuri ambao sikuwahi kuona hapa duniani.

Alichukua dakika zangu nyingi, baadaye niliamua kurudi mwanzo wa bustani ili kuanza kazi maana ndilo jambo lililokuwa limenileta ndani ya bustani hiyo ya tajiri Alexender Rugoa. Nilianza kazi yangu vema nikiupitia kila mmea kila sehemu nikihudumia kwa ustadi mkubwa, ingawa akili yangu ilikuwa imegawanyika mara mbili lakini sikuacha kufanya kazi kwa umakini na nguvu na kwa uwezo wangu wote.

Nikiwa naendelea kufanya kazi, alipita msichana mmoja mtumishi wa ndani wa hekalu hilo la tajiri Alexernder akiwa na sinia lenye matunda na vyakula vingine, alinisalimia na kunipita. Alikuwa akielekea kwa yule msichana kwenda kumpelekea chakula. Baadaye alirudi na sinia likiwa na chakula kilichobaki, aliponiona mimi nikiwa makini na kazi, alinisogelea.

“Naona kazi yako nzuri sana hakika kunapendeza,” aliongea.

Nilimtazama kwa woga fulani na kumjibu. “Asante sana.” “Naitwa Ana sijui wewe unaitwa nani?” aliniuliza.

Nilisita kidogo kumwambia jina langu lakini baadaye nilimjibu. “Naitwa Vanuell.” “Asante nimependa kukufahamu.”

“Karibu,” niliongea huku nikiendelea na kazi.”

“Unaweza kula hiki chakula? Niliyempelekea amechukua tu zabibu, siwezi kukirudisha ndani,” aliongea kwa tabasamu pana.

Nililitazama sinia lenye rangi ya dhahabu lenye matunda na keki za kisasa na kumtazama yeye usoni. Kwa kuwa nilikuwa na njaa nilitamani kula lakini haraka nilimwambia. “Samahani naomba kujua.” “Jambo gani,” aliniuliza. “Yule uliyempelekea chakula anaitwa nani?”

Alinikazia macho kwa dakika kadhaa kisha akaniambia.

“Hupaswi kujua hilo, wewe fanya kilichokuleta kakaangu.”

“Nataka kujua tu jina lake hilo tu.” “Hapana.” Aliposema hivyo aliniachia sinia la chakula pale pale na kuondoka mbele yangu, alitoka bustanini akielekea ndani ya nyumba kuu. Nilibaki nimeduwa nisielewe kitu, hakika nilibaki na maswali mengi. Nilipomaliza kufanya kazi sehemu niliyokuwa nimejipangia kwa siku hiyo, nilikaa chini na kula kile chakula kilichokuwa kimeachwa na yule msichana mzuri.

Nikiwa naendelea kula, nilishangaa kumwona msichana malaika akija kutokea kule alikokuwa, ilionyesha alikuwa akitoka eneo lake la kumpumzika akielekea ndani ya nyumba, akili yangu na viungo vyangu vilitulia huku macho yakinitoka zaidi, niliacha kula na kuganda kama sanamu. Gauni lake jeupe lililotembea hadi chini, lilimfanya aonekane malaika kweli, nilimeza mate kwa woga pindi alipokuwa akinikaribia. Nilitamani nikimbie lakini tayari alikuwa amekwishaniona.

Niliacha kula haraka na kusubiri anipite, harufu nzuri ya marashi ilianza kunijia puani kabla hata kiumbe huyo hajanifikia, mwili wangu ulianza kutetemeka kwa woga usiopimika. Baada ya dakika kadhaa alinifikia pale nilipokuwa nimekaa, jambo ambalo sikutegemea alinipita bila hata kuniambia lolote wala kunisalimia. Alizamia kwenye miti niliyokuwa nimeisawazisha na kutoka kabisa bustanini.

Nilibaki nimeduwa nisielewe kitu hapo hapo niliyakumbuka maneno ya yule dada bosi wangu kuwa msichana huyo hakuwahi kumsemesha mtu. Niliinuka pale nikiwa sijielewi vizuri, nilikusanya vifaa vyangu pamoja na lile sinia la chakula na kutoka mle bustanini, moyo wangu uliendelea kukimbia kwa maumivu makali ingawa zilikuwa zimepita dakika nyingi toka anipite.

Moja kwa moja nilitembea hadi kwenye chumba cha yule dada ambapo nilimkuta kama kawaida yake akila moshi wa sigara na kushushia na mvinyo wa bei ghali.

“Umemaliza kwa leo?” aliniuliza.

“Ndio bosi wangu nahisi kwa leo inatosha,” nilimjibu nikiwa nimekiinamisha kichwa changu chini.

Kwa mara ya kwanza aliinuka na kukaa juu ya meza kisha akanitazama sana na baadaye akaniambia.

“Sihitaji uniite dada, wala bosi.”

Nilimshangaa kidogo kisha nikamuuliza. “Nikuite nani?” “Naitwa Lucy” Nini kitaendelea? Usikose kesho.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.