SIMBA HAPA KAZI

BURUDANI - - MBELE - NA MWANDISHI WETU

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (23) akiwaongoza Donaldo Ngoma, Mbuyi Twite na Simon Msuva kumpongeza Amis Tambwe (17) baada ya kufunga bao la pili katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Prisons uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, jana. Yanga ilishinda mabao 3-0. (Pichana Emmanuel Ndege).

TIMU ya Simba imedhihirisha kile kilichosemwa na uongozi kuwa msimu huu hakuna msalie mtume, baada ya kikosi hicho kushinda mabao 2-0 dhidi ya maafande wa Mgambo JKT, mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, jana.

Mapema jana Makamu wa Rais wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kila timu watakayokutana nayo katika michuano ya ligi kuu msimu huu itawatambua kwa kipigo, jambo ambalo lilikuwa kweli katika mechi na Mgambo ambapo ulikuwa mchezo wa pili mfululizo kushinda katika jiji hilo la ‘waja leo, warudi leo’.

Simba katika mechi ya kwanza iliwakaribisha kwa kichapo cha 1-0 wageni wa ligi hiyo African Sports waliokuwa wamepotea katika ramani ya soka nchini baada ya kushuka daraja zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Katika mchezo na Mgambo JKT, Simba ilianza kwa kasi na dakika ya tatu Mohamed Hussein ‘Shabalala’ alipiga kona na mpira uliokolewa na kuwa kona nyingine ambayo haikuzaa bao.

Dakika ya sita ya mchezo huo, Peter Mwalyanzi aliwatoka walinzi wa Mgambo na kumpa pasi safi Mussa Hassan ‘ Mgosi’ aliyefumua shuti na mpira uligonga mwamba na kuokolewa.

Simba ilifunga bao la kuongoza dakika ya 26 kupitia kwa Justice Majabvi baada ya kupokea krosi kutoka kwa Tshabalala aliyekuwa amepewa pande na Mwalyanzi.

Kipindi cha kwanza Simba ilionekana kuwazidi wapinzani wao mbinu kwa kutumia viungo watano huku walinzi wa Mgambo wakimkaba zaidi Mgosi.

Wenyeji Mgambo walitumbukiza mpira katika wavu wa Simba lakini mwamuzi alikataa bao hilo kwa kuonesha ishara mfungaji alikuwa ameotea dakika chache kabla timu hizo kwenda mapumziko.

Majabvi alikosa bao dakika ya 52 baada ya Tshabalala kupiga kona na mpira kumkuta, lakini alipiga nje ya lango la Mgambo JKT.

Simba ilipata bao la pili dakika ya 73 lililofungwa na Hamis Kiiza baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Mgambo JKT.

Kiiza alifunga bao hilo la pili kwenye msimu huu akiwa na Simba ambapo awali alifunga dhidi ya African Sports katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja huo huo Jumamosi iliyopita.

Dakika 89 Kiiza alipewa kadi ya njano kwa kosa la kumvuta jezi mchezaji wa JKT Mgambo. Simba sasa ina pointi sita sawa na Yanga wanaotarajia kupambana nao Septemba 26, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Matokeo mengine ya mechi za jana, Azam FC ilifunga Stand United mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, wageni wengine wa ligi hiyo timu ya Majimaji wameendelea kutoa dozi kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, Mbeya City ilitakata 3-0 mbele ya JKT Ruvu.

Mtibwa Sugar nayo imeifunga Toto Africa mabao 2-1 katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mwadui iliibuka kidedea kwa kuichapa 2-0 timu ya African Sports ya Tanga na Ndanda FC ‘ Kuchele’ wameifunga Coastal Union bao 1-0.

African Sports na Coastal Union zimepoteza mechi mbili mfululizo tangu kuanza ligi hiyo wiki iliyopita.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.