Diamond anajua kutumia umaarufu wake

BURUDANI - - WAZO | HOJA -

KATI ya wasanii ambao siku zote sifichi hisia zangu kufunguka kwamba nawakubali, ni Nassib Abdul ‘Diamond’. Nawakubali wasanii wengi kwa ubora wa kazi zao, lakini Diamond ananikosha kwa ubunifu katika kazi zake. Anajitambua na anapiga pesa kwa akili yake.

Kutokana na Diamond kujielewa, amekuwa akitumia usanii wake kuvuna fedha nyingi tofauti na wasanii wengine wanaoishia kulewa sifa ambazo hazina maana yoyote.

Nimeshuhudia, kuandika na hata kusikia kwamba wasanii wengi nchini wamekuwa masikini wa kutupwa kwa sababu ya kutofikiria mbinu za kuvuna pesa.

Wanaimba na wakipata pesa kidogo wanajiona wamepata mabilioni. Wanaishia kulewa, kuvaa nguo za bei kali, kununua magari ya kifahari ili kuuza sura na baadaye kubaki mahututi mifukoni.

Hiyo ndio tabia ya wasanii wengi wa hapa nchini, ambao wakipewa bia za bure na kuitwa masupa staa, kwao imetosha na hawana wanachofikiria baada ya muziki nini kitafuata.

Lakini Diamond ni tofauti. Anajipambanua kutokana na ubora wa kazi zake. Anajua kujipanga katika kuachia singo zake anazotoa peke yake au kushirikiana na wasanii wa ndani na wale wa nje ya nchi.

Kupitia singo moja tu amekuwa akiingiza fedha nyingi kwa maonyesho ya ndani na nje ya nchi, pia wimbo huo huo hununuliwa na kampuni ya simu za mikononi kwa ajili ya milioni.

Akili hiyo inamsaidia kupata pesa nyingi na sasa amekuja na wazo jipya ambalo mara nyingi najua linafanywa na wasanii wengi wa Marekani au Ulaya, la kuuza haki za sura ya mtoto wake, Princess Tiffah.

Diamond kupitia

akaunti yake ya Instagram iitwayo princess_tiffah aliweka sura ya mtoto huyo baada ya kukubaliana na benki moja nchini kudhamini sherehe ya kutimiza siku 40 tangu kuzaliwa mtoto huyo, ambaye tayari ana mkataba na maduka mawili ya nguo za watoto.

Msanii huyo ambaye amezaa na Zarinah Hussein, amekuja na mfumo huo mzuri wa kupata pesa ambao haikuwa kawaida kufanywa na wasanii wa Afrika, hasa Tanzania.

Hivyo ni wakati wa wasanii wote kujifunza kitu kutoka kwa Diamond, ambaye anastahili kila sifa kutokana na kupambana kubaki juu na kupuuza wanaomchukia.

Funzo mojawapo ambalo naliona kutoka kwa Diamond ni wasanii wenzake kutambua thamani yao kwani wakijielewa watafanya kama alivyofanya, kuuza haki za picha za mtoto wake na kujiongezea fedha katika akaunti yake.

Wasanii wengi wamekuwa wakijifungua na kuweka picha za watoto wao katika mitandao ya kijamii bila ya kufikiri kuwa zina thamani kama wakijenga ushawishi wa kuuza haki hizo kwenye majarida na magazeti mbalimbali.

Lakini kusambaza picha hizo katika mitandao na kudhani zinawaongea umaarufu ni kujidanganya. Wanafikiri ujiko unazidi wakati wapo taabani kifedha.

Umefika wakati kila msanii ajiulize thamani yake na kubuni mbinu za kuchota ‘mihela’ kuliko kusubiri dhiki baada ya kazi ngumu majukwaani.

Safi Diamond kwa kujaaliwa kipaji cha kuimba na kujiongezea kipato kwa njia nyingine kama hiyo ya kuuza haki za sura ya Princess Tiffah.

Kwangu anabaki kuwa msanii wa kuigwa, ingawa akumbuke kutunza ‘mpunga’ wake vizuri kwani kuna maisha baada ya sanaa.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.