LUNYAMILA KUCHEZA SOKA ITALIA

BURUDANI - - MBELE -

WAKATI klabu ya Simba inakamilisha mipango ya kumsajili winga machachari Edibily Lunyamila, kuna mipango mingine inafanyika ili kwenda kucheza kwa majaribio nchini Italia.

Lunyamila aliyechukuliwa msimu uliopita na timu ya Malindi ya Zanzibar kutoka Yanga ya Dar es Salaam pamoja na wachezaji wote wanaotoka nje ya Zanzibar, mikataba yao imesitishwa na timu hiyo ya Malindi.

Mipango ya kwenda kucheza nje inafanywa na mwanamichezo John Lamba ili aende Italia kwa majaribio ya miezi mitatu katika klabu moja ya daraja la kwanza ambayo haikuweza kufahamika.

Lamba ni mwanachama wa klabu ya Simba na mmoja wa wafadhili wa klabu hiyo, anafanya mipango kwa ushirikiano na watu wa nje ya nchi wanaokamilisha mipango hiyo ya kumpeleka Lunyamila nchini Italia.

Pamoja na mipango hiyo kufanywa bado hakuna uhakika timu ipi Lunyamila atapata nafasi ya kujaribiwa na iwapo ataweza kukabiliana na hali ya hewa ya huko atapaokuwa akicheza.

Imeelezwa kuwa mipango hiyo inalingana kwa kiasi fulani na ile aliyofanyiwa Athuman China alipokwenda Uingereza kwa majaribio ya kucheza soka ya kulipwa. Mipango hiyo ilifanywa chinichini kwa ushirikiano wa Lamba na mzungu mmoja ambaye jina lake halikufahamika.

Iwapo Lunyamila atafanikiwa kuvuka majaribio kwa kiwango kinachotakiwa atasaini mkataba wa muda mrefu kucheza mpira wa kulipwa nchini humo.

Italia ni moja ya nchi za Ulaya zinazochukua wachezaji wengi kutoka Afrika, hasa Afrika Magharibi na akifanikiwa atakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika Mashariki na Kati.

Lamba alipoulizwa alisema kuwa hafahamu mipango hiyo ila aliambiwa na mzungu huyo ambaye ni rafiki yake wa karibu pia wakala wa wachezaji, kutafuta wachezaji wenye kiwango cha juu kutoka Afrika Mashariki kwenda kucheza mpira wa kulipwa Italia.

Pamoja na kutakiwa kwenda kucheza mpira wa kulipwa kuna habari kuwa Lunyamila amekamilisha mipango ya kujiunga na klabu ya Simba ya Dar es Salaam kwa ajili ya msimu ujao wa ligi daraja la kwanza.

Timu ya Simba ilikuwa ikimwinda kwa muda mrefu mchezaji tangu yupo klabu yake ya zamani Yanga kabla ya kuchukuliwa na Malindi ya Zanzibar.

HUO ULIKUWA MWAKA 1995.

LUNYAMILA

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.