‘Hakuna dhambi Mkwasa kupewa mkataba Stars’

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumpa Charles Boniface Mkwasa, mkataba wa miaka miwili wa kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars siyo dhambi.

Yanga imesema hawana pingamizi lolote kwa TFF, kumpatia kocha huyo msaidizi wa mabingwa hao wa soka nchini, mkataba wa kudumu wa kuinoa Taifa Stars, kwa vile amekwenda kuitumikia nchi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, alisema uamuzi huo wa TFF ni sahihi kwa vile Mkwasa anavyo vigezo vyote muhimu vya kuwa kocha wa timu ya taifa.

Alisema Yanga inaona fahari kubwa kwa Mkwasa kupata mkataba wa kudumu wa kuinoa Taifa Stars ili aweze kuelekeza nguvu zake kwenye kikosi hicho.

“Sisi hatuna pingamizi. Unajua mara nyingi amekuwa hatulii,mara yupo Yanga, mara anakwenda Taifa Stars. Sasa amepata kazi ya kudumu, hakuna dhambi yoyote,” alisema Muro.

Kauli hiyo ya Muro, imekuja siku chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza rasmi kumpa mkataba huoMkwasa, ambao umeanza rasmi Oktoba Mosi, mwaka huu, na utamalizika Machi 31,2017.

Awali, kocha huyo alipewa jukumu la kuinoa timu hiyo kwa muda mfupi wa miezi mitatu kabla ya TFF kuukubali uwezo wake na kuamua kumpa mkataba wa kudumu.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.