Wachezaji Yanga, Azam chini ya ulinzi

BURUDANI - - HABARI - NA MWANDISHI WETU

WACHEZAJI wa timu za soka za Yanga na Azam FC, waliopo kwenye kambi ya timu ya taifa,Taifa Stars, wamewekwa chini ya ulinzi mkali wa manahodha wa timu hizo.

Uchunguzi uliofanywa na Burudani juzi na jana, umebaini kuwa wachezaji wa Yanga, walioweka kambi kwenye Hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, wapo chini ya uangalizi wa nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Nahodha huyo amepewa jukumu la kuangalia mwenendo mzima wa wachezaji wenzake wa timu hiyo, kabla ya mchezo wa jana dhidi ya timu ya taifa ya Malawi, The Flames.

Mechi hiyo ilikuwa ya kuwania kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia, ambazo zitafanyika 2018 nchini Russia.

Wachezaji wengine wa Yanga, waliopo kwenye kikosi hicho ni Ali Mustapha, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondan, Salum Telela na Deus Kaseke.

Kwa upande wa Azam FC, jukumu la kuwalinda wachezaji wao amekabidhiwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’.

Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa, lengo ni kuhakikisha wachezaji hao hawarubuniwi kabla ya mchezo kati ya Yanga na Azam wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Oktoba 17, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji wa Azam waliopo Taifa Stars ni Aishi Manula, Shomari Kapombe,Himid Mao, Mudathir Yahaya, Frank Domayo, Farid Musa, na Bocco.

Newspapers in Swahili

Newspapers from Tanzania

© PressReader. All rights reserved.